Habari za Punde

ZITTO KABWE AUSHUKURU UBALOZI WA CHINA NCHINI TANZANIA

Kwa niaba ya Manispaa ya Kigoma Ujiji naomba kuchukua fursa hii kuushukuru Ubalozi wa China nchini, Balozi pamoja na Timu ya Wawekezaji kutoka China waliokuwa wageni wetu hapa Ujiji kwa muda wa siku 3. 
Ujio wao ni jambo lenye faraja kwetu kwamba juhudi zetu za kuainisha fursa za uwekezaji hapa Kigoma (kupitia mwongozo wa Uwekezaji Kigoma Ujiji - Kigoma Ujiji Investor's Guide) zimeanza kuzaa matunda na kuvutia uwekezaji kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Ziara ya Balozi Lu Youqing na timu yake imewezesha makubaliano kwenye maeneo matano (5) ya uwekezaji:
1. Ujenzi wa Kiwanda cha kuchakata Samaki na mazao ya Samaki katika mji wa Katonga, Kata ya Bangwe.
2. Ujenzi wa Kituo cha Biashara Ujiji (Ujiji City - The Great Lakes Trade and Logistics Center) katika kata ya Kitongoni na Kasimbu.
3. Uwekezaji Wa Kiwanda cha kusindika mazao ya michikichi.
4. Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Vijana eneo la Mwanga Community Center.
5. Ukarabati wa Soko la Ujiji na jengo la watumwa na ujenzi wa barabara ya watumwa ili kukuza Utalii na Ujenzi Mwalo wa Katonga.
Ziara ilikuwa ya mafanikio makubwa sana, ikitufikisha hata katika maeneo ambayo ni nadra mabalozi kufika (kama pichani tukivuka mto Luiche), ninaamini kuwa wananchi wa Kigoma watafanikiwa na miradi hii inayotokana na mahusiano mazuri kati ya nchi yetu na Jamhuri ya watu wa China. 
Ni dhamira yetu kuhakikisha tunautumia muda wa dhamana yetu tuliyopewa na wananchi kushirikiana nao kuleta maendeleo na kuipeleka mbele Kigoma Ujiji.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge, Kigoma Mjini - ACT Wazalendo 
Kigoma

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.