Habari za Punde

BONDIA MAYWEATHER KULETWA NCHINI NA PROMOTA JUMA NDAMBILE

Na Ripota wa Mafoto Blog, Dar 
Promota  na meneja maarufu wa ngumi za kulipwa nchini, Juma “Chief” Ndambile  yupo katika mikakati ya kumleta nchini bondia maarufu wa ngumi za kulipwa Duniani, Floyd Mayweather Jr mara baada ya pambano lake Conor McGregor.
Awali, Mayweather alipanga kutembelea Ghana mwezi  Juni, lakini safari hiyo iliharishwa ili kujiandaa na pambano lake dhidi ya bondia McGregor  lililopangwa kufanyika Agosti 26 kwenye  Las Vegas' T-Mobile Arena.
Ziara ya Ghana kwa bondia huyo imeandaliwa na kampuni ya Upscale Entertainment ambapo mbali ya Ghana, bondia huyo alipanga kutembelea Nigeria.
Ndambile alisema jana kuwa amefanya mawasiliano na waandaaji wa ziara ya bondia huyo nchini Ghana na mazungumzo yanaendelea vizuri.  Ndambile alisema  baada ya kufanya mazungumzo ya awali, alilazimika kusafiri hadi Ghana ili kujadiliana jinsi ya kufanikisha ziara hiyo.
“Nilikwenda Ghana na kukutana na waratibu wa ziara hiyo, kuna mambo ambayo tulikubaliana nao kuhusiana na ziara hiyo, tunaendelea vizuri sana, tunasubiri pia menejimenti ya bondia huyo kutangaza tarehe rasmi ya kufika 
Ghana na masuala mengine yatafuatia,” alisema Ndambile.
Ndambile alisema kuwa  ameweka nia ya kufanikisha yale aliyoyapanga  mara baada ya kuhudhuria mkutano mkuu wa Baraza la Ngumi za Kulipwa Duniani (WBC) uliofanyika Desemba 11-17 Marekani. Tayari promota huyo amekabidhi taarifa ya mipango yake ya kuendeleza ngumi za kulipwa kwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe.
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe akiangalia  ripoti ya promota wa ngumi za kulipwa nchini na Mkurugenzi wa Kampuni ya Advanced Security, Juma Ndambile mara baada ya kumkabidhi hivi karibuni.
***************************************************
“Nikiwa Marekani, niliweza kukutana na Rais wa WBC, Mauricio Sulaimai pamoja na bondia Mayweather, mabondia Lenox Lewis, Amir Khan, Wladimir Klitschko, Evander Holyfield na mapromota maarufu kama Don King na Jay Mathews, wote hao wameonyesha nia ya kuja nchini kwa ajili ya kuona vivutio vya utalii na kuwekeza,” alisema Ndambile.
Alifafanua kuwa ameamua kuwekeza katika mchezo huo na amaani endapo atafanikisha ujio wa Mayweather, Tanzania itapaa katika mchezo wa ngumi za kulipwa na vile vile kutangaza utalii.
Promota wa ngumi za kulipwa nchini, Juma “Chief Ndambile” akiwa katika picha ya pamoja na promota maarufu wa ngumi za kulipwa Duniani,  Don King mara baada ya kukutana kwenye mkutano wa WBC nchini Marekani.
Promota wa ngumi za kulipwa nchini, Juma “Chief Ndambile” akiwa katika picha ya pamoja na bondia maarufu wa zamani wa ngumi za kulipwa Duniani, Evander Holyfield mara baada ya kukutana kwenye mkutano wa WBC nchini Marekani 
Promota wa ngumi za kulipwa nchini, Juma “Chief Ndambile” akiwa katika picha ya pamoja na bondia maarufu wa ngumi za kulipwa wa zamani, Lenox Lewis mara baada ya kukutana kwenye mkutano wa WBC nchini Marekani.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.