Habari za Punde

LIVE: KUTOKA DODOMA, WAZIRI MWAKYEMBE AFUNGUA MKUTANO MKUU WA TFF DODOMA

 Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, akizungumza na wajumbe wa Mkutano mkuu wa TFF, wakati akifungua rasmi mkutano huo kwenye Ukumbi wa Hoteli ya St. Gaspa mjini Dodoma leo Agost 12, 2017. Picha na Muhidin Sufiani (MAFOTO)
**************************************
Na Ripota wa Mafoto Blog, Dodoma
SERIKALI imesema itamburuza mahakamani kiongozi yeyote wa Shirisho la Soka Tanzania (TFF), atakayebainika kuwa ameingia 
madarakani kwa kutumia rushwa. 
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Ofisa Mkuu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Dodoma, Mussa Chauli, 
alipokuwa akitoa nasaha kabla ya kuanza uchaguzi. 
Uchaguzi Mkuu wa TFF ulifanyika jana kwenye Ukumbi wa St Gasper nje kidogo ya mji wa Dodoma ambapo Wajumbe wa Mkutano 
Mkuu walichagua viongozi ambao watakuwa madarakani kwa miaka minne. 
Chauli alisema TAKUKURU inafuatilia kwa karibu uchaguzi huo na aliwataka wagombea wote kuacha kutumia rushwa kwa wajumbe 
kwa kuwa ni kosa la kisheria. 
Alisema uzoefu unaonyesha wagombea wengi wanaotaka madarakani katika taasisi hiyo wamekuwa wakitumia rushwa na serikali 
itakuwa makini kufuatilia nyendo za kila mgombea. 
Chauli alisema baada ya uchaguzi kufanyika, taasisi hiyo itaendelea kufuatilia kwa karibu mchakato mzima wa uchaguzi na 
TAKUKURU ikibaini kuna kiongozi aliingia madarakani kwa kutumia rushwa atang'olewa. 
"Natoa onyo kwa mgombea yoyote ambaye ataingia madarakani kwa kutumia rushwa, tutaishauri serikali kumfungulia mashitaka 
ya rushwa na atafikishwa kwenye vyombo vya sheria," alisema Chauli. 
Alisema vitendo vya rushwa TFF imeota mizizi, lakini TAKUKURU itakuwa macho kuhakikisha wagombea wote wanashinda kwa 
haki kwa mujibu wa katiba. 
 Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano mkuu na wagombea katika Uchaguzi mkuu wa TFF, katika ukumbi wa St. Gaspa mjini Dodoma.
***********************************
"Tutaishauri serikali kuchukua hatua endapo tutabaini kuna kiongozi ameingia madarakani kwa kutumia rushwa, tutamuondoa 
mara moja na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi," alionya Chauli. 
Chauli alisema sekta ya michezo imegubikwa na rushwa, hivyo serikali itakuwa makini kufuatilia nyendo za kila mgombea na 
aliwataka wajumbe kuwa makini. 
Alisema baadhi ya vitendo vya rushwa vinavyoitafuna TFF ni upangaji wa ratiba, udhibiti wa mapato na matumizi, kupeana 
rushwa kwa viongozi na wajumbe. 
Naye mgeni rasmi Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe, alisema kwa mara ya kwanza katika 
historia ya nchi viongozi watakaochaguliwa wataapa kwa msajili mbele ya wajumbe. 
Alisema lengo la kutaka kila mgombea kuapa kwa msajili inatokana na ukweli kwamba viongozi wengi wanaoingia madarakani 
wamekuwa wakiingia madarakani kwa kutumia rushwa. 
 Baadhi ya Wajumbe wa mkutano huo
*******************************************************
"Mgombea yeyote ambaye amechukua fomu ya kuwania uongozi kwa kutumia rushwa au anatafuta uongozi ili kujipatia fedha 
huyo atakuwa amepotea,"alisema Dk. Mwakyembe. 
Dk. Mwakyembe aliwataka Wajumbe wa Mkutano Mkuu kutokufanya makosa katika uchaguzi huo kwa kuwa serikali ina dhamira ya 
dhati ya kuendeleza soka nchini. 
Alisema serikali inataka kufanya kazi na viongozi waadilifu ambao wameshinda kwa uhalali bila kuwa na harufu ya rushwa, 
hivyo aliwataka wajumbe hao kuwa makini katika uamuzi wa kuchagua viongozi wa TFF. 
Waziri huyo alisema Watanzania wana matumaini makubwa wajumbe watachagua viongozi makini bila ushawishi wa rushwa ili 
kuleta mageuzi ya soka. 
 Makamu wa Rais wa TFF, Wallase Karia, akizungumza katika mkutano huo.
*******************************************
Alionya wajumbe kuwa wamebeba dhamana kubwa katika sekta ya michezo na aliwataka watende haki kwa kuchagua viongozi bora 
ambao watakuwa na manufaa kwa taifa. 
"Tunataka viongozi ambao wataisimamia Serengeti Boys ili iweze kushiriki mashindano ya olimpiki ya vijana. Tunataka 
viongozi watakaoshirikiana na serikali kuwaendeleza vijana waliopatikana kutoka katika michezo ya UMISETA,"aliongeza Dk. 
Mwakyembe. 
Pia alisema serikali itaendelea kuheshimu uhuru wa vyama vya michezo nchini, lakini haitavumilia viongozi wazembe ambao 
watakuwa wabadhirifu. 
Katika uchaguzi huo ulioanza saa 6:42 kwa wagombea wa nafasi ya ujumbe kujinadi, ulitumia dakika mbili kwa kila mmoja 
kuomba kura kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF. 
Saa 7:43 wagombea wa nafasi ya Makamu wa Rais walianza kujinadi kwa kutumia dakika tatu ambapo alianza Mlamu Nghambi, 
Michael Wambura, Mtemi Ramadhani na Robert Selasela. Aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo Steven Mwakiborwa juzi aliandika 
barua ya kujitoa. 
 Mwakilishi wa CAF, Veron akizungumza kutoa salamu zake kutoka CAF
**********************************************
Wagombea wa nafasi ya urais walipewa dakika tano kila mmoja kujinadi na pazia lilifunguliwa na Imani Madega saa 7:56 
akifuatiwa na Wallace Karia, Frederick Mwakalebela, Ali Mayay, Shija Richard na Emmanuel Kimbe. 
Katika hali isiyotarajiwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya ujumbe aliwaacha hoi wajumbe na viongozi mbalimbali ndani ya 
ukumbi baada ya kudai alichelewa kujinadi kwa kuwa alipatwa ghafla na tumbo la kuharisha. 
"Ni kweli nimechelewa kuja kujinadi kwa sababu ya dharura ya tumbo iliyonipata, haikuwa dhamira yangu ni mambo ya Mungu 
yeye ndiye mpangaji wa yote," alisema Ali Kamtande kutoka Kanda ya Dar es Salaam. 
Pia mmoja wa wagombea wa nafasi ya ujumbe kutoka Mkoa wa Katavi, alishindwa kutaka vyama vinne vya michezo ndani ya mkoa 
wake hatua iliyoibua mayowe ndani ya ukumbi. 
 Rais wa Shirikisho la Soka Djibout, Suleiman Wabere, akitoa salamu zake wakati wa mkutano huo.
***********************************************
Ndani ya ukumbi wa mkutano na maeneo jirani ulinzi mkali uliimarishwa kuanzia getini ambapo kila mtu aliyekuwa akiingia 
alikaguliwa kwa kutumia mashine maalumu. 
Hali ndani ya viunga vya ukumbi ulikuwa shwari na kila mtu alikuwa makini huku maofisa wa usalama na TAKUKURU wakichukua 
nafasi zao kuhakikisha hakuna vitendo vya rushwa vinavyoweza kutokea. 
Wakati huo huo, mtu mmoja alikamatwa ndani ya maeneo ya ukumbi akiwa na fedha zinazodaiwa ziliandaliwa kuwapa baadhi ya 
wajumbe wa mkutano mkuu. 
Kauli hiyo ilitolewa na Ofisa Usalama Viwanjani anayetambuliwa na FIFA Hashim Abdallah, alipokuwa akitoa taarifa kuhusu 
hatua zilizochukuliwa kuhakikisha vitendo vya rushwa vinakomeshwa katika uchaguzi.
 Benchi la kujiandikisha wajumbe
 Wajumbe...
 Meza Kuu
 Wajumbe
 Wajumbe wakijitambulisha
 Wajumbe
 Muonekano wa ukumbi huo
 Meza ya wawakilishi wa CAF
 Meza kuu
 Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe,akiagana na baadhi ya wajumbe wa mkutano huo na wawakilishi wa CAF baada ya kufungua rasmi.
WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe,akiagana na Makamu wa Rais wa TFF Walles Karia.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.