Habari za Punde

MSD NA ZIPLINE WASAINI MKATABA WA NDEGE ZISIZO NA RUBANI KUSAMBAZA DAWA NA VIFAA TIBA

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Laurean Bwanakunu (kushoto), akibadilishana hati za mkataba na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Zipline, Keller Rinaudo, jijini Dar es Salaam jana, baada ya kutiliana saini makubaliano ambapo kampuni hiyo itaanza kusambaza dawa katika maeneo yasiyofikika kwa kutumia ndege zisizo na rubani. Katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya.
*************************************
Na Ripota wa Mafoto Blog, Dar
SERIKALI imeingia makubaliano na Kampuni ya ZIPLINE ya nchini Marekani kwa ajili ya usambazaji wa dawa,damu, vifaa tiba na nyaraka kwa kutumia ndege zisizo na rubani.
Makubaliano hayo ambayo yatasimamiwa na Bohari ya Dawa (MSD) yameweka historia kwa Tanzania kuwa nchi ya pili Barani Afrika katika kutumia hudumu hiyo lengo likiwa ni kuboresha sekta ya afya na kuwafikia wananchi wa pembezoni kwa wakati.
Akizungumza jana katika makubaliano hayo jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dk. Mpoki Ulisubisya, alisema mpango huo wa usambazaji wa dawa kwa ndege zisizo na rubani utaboresha sekta ya afya na kupunguza vifo visivyo na lazima.
Alisema katika mpango wa serikali kuongeza bajeti ya dawa kwa mwaka wa fedha umesababisha kuwa na mahitaji makubwa ambapo vituo vya serikali zaidi ya  5640 vinategemea MSD.
"Vituo hivyo ni nje ya vya taasisi za dini,kijamii na vya watu binafsi ambavyo tumeingia nao makubaliano hivyo uhitaji ni mkubwa na huduma hii itafikia malengo,"alisema.
Dk. Mpoki alisema ndege hizo ambazo zitasambaza dawa,vifaa tiba,damu na nyaraka muhimu na kutua sehemu zilizokusudiwa kisha kusambazwa zitawafikia wananchi wengi wa pembezoni.
Alisema ndege hizo nyingi zinatumika vitamika ba baadhi ya nchi katika  kuokoa maisha ya watu na serikali imeona haja ya kuzitumia katika kuokoa maisha ya watanzania  katika sekta ya afya.
"Wengi tunatambua tatizo kubwa walilonalo wakina mama wakati wa kujifungua hivyo teknolojia hii itakuwa ni mkombozi katika kuwapatia wananchi huduma kwa wakati,"alisema.
Alihimiza haja ya wataalamu wa ndani kushirikishwa ili kuwa na uzoefu katika teknolojia hiyo na kupunguza changamoto za kiutendaji.
Alisema mradi huo utaanzia Mkoa wa Dodoma na gharama zake zitalipwa na wahisani.
Alisema Tanzania imeweka historia kutokana na mradi huu na kuwa nchi ya pili barani Afrika ikifuatiwa na Rwanda katika kutumia teknolojia hiyo kuboresha huduma za afya.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ZEPLINE,Keller Rinaudo alisema imekuwa ni kawaida kwa nchi kama Tanzania kuiga teknolojia muhimu kama hiyo kwa nchi za Afrika lakini kwa sasa ni wazi nchi hizo zitaiga mafanikio yatakayofikiwa nchini.
 Rinaudo alikubaliana na ombi la serikali la kuona haja ya teknolojia ya uzalishaji wa ndege hizo kufanyika ndani ya nchi na kuahidi kufanyia kazi hatua hiyo.
Alisema anamini uongozi wenye nia dhahiri ya kuleta mabadiliko uliopo nchini hivyo amewahakikishia watanzania kuwa mradi huo utakuwa chachu katika sekta ya ajira kwa wazawa watakaokuwa tayari kujifunza na kufanya kazi naye kwa uadilifu.
"Ndege hizo zitakuwa zinatumia dakika 10 kufikisha mizigo na  kubeba  kwa safari moja kilogram 1.8 na uwezo wa kusafiri kilomita 150 kwenda na kurudi,"alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa MSD Laurean Bwanakunu alisema Taasisi hiyo itaanza kusambaza dawa hizo kwa mfumo uliokusudiwa mapema mwakani. 
Alisema kutokana na makubaliano hayo MSD itashirikiana na Ifakara Institute katika kufanya tafiti na kubaini mahitaji yaliyopo katika maeneo.

Alisema wanatarajiwa baada ya mwaka mmoja kuwafikia wananchi waliopo mikoa 10 ikiwemo Kanda ya Ziwa ,Nyanda za juu Kusini,Pwani hususani Tanga na wananchi milioni 10 watapata huduma hizo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.