Habari za Punde

PLUIJM: YANGA ITAIFUNGA SIMBA NGAO YA JAMII

KOCHA mkuu wa Singida United, Hans Pluijm ameitabiria timu ya Yanga kuwa itapata ushindi dhidi ya Simba katika mechi ya mchuano wa Ngao ya Jamii.

Yanga itachuana na Simba katika mechi hiyo iliyopangwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Pluijm alisema kuwa Yanga ina kikosi cha wachezaji wengi wazawa na wazoefu ambao wanaweza kuamua mechi hiyo kuliko Simba.

Alisema Yanga ina wachezaji wengi vijana ambao wanaweza kubadili mchezo huo kuliko Simba ambao hawana kikosi mbadala baada ya kile cha kwanza kilichokuwa na wachezaji wenye umri mkubwa.

Alisema timu zote zimefanya usajili mzuri katika kipindi hiki cha usajili lakini Yanga imefanikiwa kutibu tatizo lake la kiungo mkabaji hivyo inaweza kupata ushindi katika mechi hiyo.

Pluijm ambaye aliwahi kuinoa klabu hiyo alisema Simba imesajili wachezaji wengi wa kigeni hivyo itachukua muda mrefu kuzoeana na kufanya vyema ambapo Yanga itakuwa na nafasi kubwa ya kuwafunga wekundu wa msimbazi hao.

Wakati huo huo kocha huyo alisema kuwa kikosi chake kimeshaanza kuzoeana kwa kuwa alikuwa na wachezaji wengi wakigeni hivyo atahakikisha analeta ushindani katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu ujao.

Alisema kikosi chake kina wachezaji wengi wa kigeni na wazoefu hivyo itasaidia kupambania ubingwa wa ligi na kufanya mapinduzi katika timu za Simba na Yanga.

Singida United imepanda katika ligi kuu msimu huu baada ya kucheza kwa mafanikio makubwa kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu uliopita na kuongoza kundi lao.

Timu hiyo inatarajia kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Yanga kesho katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya ligi kuu msimu ujao.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.