Habari za Punde

SERIKALI YAAGIZA UCHUNGUZI KUHUSU CHANZO CHA KUUNGUA KWA JENGO LA FDC -SIKONGE.

Na Tiganya Vincent, RS-TABORA
SERIKALI imeuagiza Uongozi wa Wilaya ya Sikonge kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuchunguza chanzo cha moto katika Jengo la Utawala la Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Sikonge ambao ulisababisha hasara inayozidi shilingi milioni 24. 
Agizo limetolewa jana wilayani Sikonge na  Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Mhandisi Stella Manyanya  wakati alipotembelea Chuo hicho kujionea athari zilizotokana na moto huo.
Alisema kuwa ni vema Kikosi cha Zimamoto kwa kushirikiana vyombo vingine kikasaidia kuchunguza chanzo cha moto ili kama kuna hujuma wahusika wote waweze kuchukuliwa hatua mbalimbali za kisheria.
Mhandisi Manyanya alisema kuwa matukio ya moto katika maeneo mbalimbali yamekuwa yakirudia rudia na kutia shaka kuwa vitendo vya aina hiyo vimekuwa vikifanywa makusudi ili wahusika wapate kujengewa jengo jingine au wakati mwingine kutaka kupoteza baadhi ya ushahidi kuhusu baadhi ya makosa yao. 
“Nimesikitika sana wakati napanga kuja huku kuona Chuo kwa Mwaliko wa Mbunge wa Sikonge Usiku wake Jengo la utawala linaungua….mimi sijafurahia ni vema uchunguzi wa kina ufanywe kuja chanzo na nipate taarifa” alisema Manyanya.
Aliagiza kuwa kunapoteka moto ni vema uchunguzi wa kina ukafanyika badala ya kusingizia itirafu ya umeme kama ndio chanzo cha umeme.
Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa haiwezekani Serikali inatoa fedha nyingi  kwa ajili ya ujenzi wa majengo mbalimbali kwa shughuli za maendeleo kisha muda si mrefu unakuta limeungua na kisingizio ni umeme.
Aidha aliuagiza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge kutumia fedha zao kujenga upya jengo hilo lilioungua na wala wasitegemee fedha kutoka Wizara ya Elimu.
Alisema kuwa Wizara itasaidia katika ukarabati wa majengo mengine na sio kujenga jengo hilo lililounguzwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Peres Magiri alisema kuwa moto huo ulitokea majira ya saa 7 usiku na kusababisha hasara iliyotokana na uharibifu wa jengo na wizi uliofanywa na baadhi ya watu waliojifanya kusaidia kuzima moto huku wakipora baadhi ya vitu.
Alisema kuwa katika tukio hilo hakuna mtu aliyepata majeruhi yaliyotokana na moto huo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.