Habari za Punde

TFF YAMTOA 'JELA' CHIRWA NA WENZAKE, MSUVA AONYWA

Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), chini ya Makamu Mwenyekiti, Peter Hellar ilikutana jana Jumatano Agosti 30, mwaka huu ikiwa na ajenda kuu ya mashauri yanayohusu wachezaji watatu.
Wachezaji hao ni Obrey Chirwa wa Young Africans pamoja na wenzake wawili Deus Kaseke na Simon Msuva ambao kwa pamoja msimu uliopita walikuwa wanaitumikia klabu hiyo ya Jangwani.
Wachezaji hao walisimamishwa kucheza soka katika uamuzi uliofanywa na Kamati ya 72 ya Bodi ya Ligi kwa mujibu wa kanuni ya 9 (5) ya Ligi Kuu kutokana na kumvamia na kumsukuma mwamuzi Ludovic Charles aliyechezesha mechi ya Young Africans na Mbao Mei 20, mwaka huu.
Kati ya watuhumiwa wote, Kamati ilimtia hatiani Simon Msuva na kuwaachia huru Deus Kaseke na Obrey Chiwa. Msuva alionekana kumvamia na kumwangusha mwamuzi kinyume cha kanuni ya 49 (1) (b) ambapo sasa anatakiwa kusimama mechi tatu za aina yeyote ya mashindano ya ndani.
Kwa mujibu wa Wakili Hellar tayari Msuva alikosa mechi za mashindano ya Sportpesa hivyo Kamati imetambua kwamba tayari ametumikia adhabu husika, lakini inampa onyo kali la maandishi kwa mujibu wa kanuni ya 14.
Kamati imeshauri TFF na Bodi ya Ligi ni vvema kuachia Kamati majukumu ya kusimamisha na kufungia kwa mujibu wa kanuni za kinidhamu badala ya taasisi hizo kuchukua hatua ya kusimamisha ambazo hazileti haki na usawa uwa ni kama adhabu.

Ushauri huo umepokelewa na TFF na itaufanyia kazi.
Itakumbukwa kwamba mechi iliyowaletea shida wachezaji hao ni namba 236 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Yanga ikipoteza kwa bao 1-0.
Mara baada ya mchezo huo, Kamati ya 72 ya Bodi ya Ligi ilipitia matukio mbalimbali na kufikia uamuzi wa kuwasimamisha wachezaji Deus Kaseke, Simon Msuva na Obrey Chirwa wa Yanga kucheza mechi za Ligi Kuu.
Walisimamishwa wakisubiri suala lao la kumsukuma na kumwangusha Mwamuzi Ludovic Charles kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Wachezaji hao walidaiwa kufanya kitendo hicho katika mechi hiyo dhidi ya Mbao FC iliyofanyika Mei 20, 2017 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijni Mwanza. Uamuzi wa Kamati ya Saa 72 ulizingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu. 
Itakumbukwa, Mwamuzi Ludovic Charles amepewa onyo kali kwa kutodhibiti vizuri mchezo. Uamuzi dhidi yake ni kwa mujibu w Kanuni ya 38(5) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.