Habari za Punde

TUNATAKA UADILIFU LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA BARA

LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), msimu wa 2017/18 inaanza rasmi kesho Jumamosi Agosti 26, 2017 kwa michezo saba itayochezwa katika viwanja tofauti nchini.
Ni msimu mpya wenye Viongozi wapya wa shirikisho la mpira wa miguu wapya ,utakaotoa timu bingwa mpya itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika inayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), msimu wa 2019.
Itakumbukwa, msimu wa CAF wa 2018, timu itakayoiwakilisha nchi ni Young Africans SC ambayo ni Bingwa wa VPL msimu 2016/17 wakati michuano ya Kombe la Shirikisho, Tanzania itawakilishwa na Simba SC.
TFF tunazitakia kila la kheri timu zote zinazoshiriki ligi hii, tukiamini kwamba uadilifu utaongoza mbele ya taratibu, kanuni na sheria zinazosimamia mpira wa miguu hapa nchini na kwingineko.
Kwa mechi za kesho Jumamosi, Simba inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wakati Mbao watakuwa wageni wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Mchezo mwingine utakuwa ni kati ya Majimaji ya Songea itakayosafiri hadi Mbeya kucheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini humo huku Njombe Mji ikiialika Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Sabasaba huko Makambako.
Kadhalika Uwanja wa Manungu ulioko Turiani, Mtibwa mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar itaikaribisha Stand United ya Shinyanga kwenye mchezo mwingine wa VPL ilihali Azam atakuwa mgeni wa Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara. 
Mwadui watakuwa wenyeji wa Singida United ya Singida kwenye Uwanja wa Mwadui huko Shinyanga na Jumapili kutakuwa na Mchezo mmoja utakaokutanisha Young Africans na Lipuli kwenye Uwanja wa Uhuru jijini.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.