Habari za Punde

WANA CCM WA KATA YA MZINGA KUKUTANA JUMAPILI


Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mzinga, Majaliwa (kulia) akipongezwa na mmoja wa Wanachama wa CCM baada ya kutangazwa kuchaguliwa kuwa nwenyekiti wa Kata hiyo, hivi karibuni
******************************************
Na Ripota wa Mafoto Bolg, Dar
MKUTANO Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mzinga wilayani Ilala, Dar es Salaam, unatarajiwa kufanyika Jumapili wiki hii.

Katibu Mwenezi wa CCM wa kata hiyo Paul Kapotele, amesema wajumbe wameshataarifiwa kuhudhuria mkutano huo wa kuwatambulisha viongozi wapya pamoja na kuwashukuru wapigakura.

Alisema mkutano huo umepangwa kuanza saa 5:00 asubuhi katika ukumbi wa Mkwabi, ambapo pia viongozi wa zamani wa CCM na makada mbalimbali wamealikwa.
"Viongozi wapya tulichaguliwa Agosti 5 mwaka huu kwa hiyo tumeona ipo haja ya kuita tena Mkutano Mkuu ili kuwashukuru wapigakura kisha hapo tuanze kuchapakazi," alisema Kapotele.
Alisema malengo ya uongozi mpya ni kukipa ushindi Chama katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka 2019 na uchaguzi mkuu.
"Baada ya kumalizika uchaguzi tuliangalia namna ya kuimarisha uhusiano kati ya viongozi na wanachama ndio maana tumeandaa mkutano huu kwa lengo la kujenga," alifafanua Kapotele.
Alisema kuwa ana imani baada ya mkutano huo, CCM Mzinga itakuwa imara kufuatia upendo na umoja utakaojengeka miongoni mwa wanachama, viongozi na wapenzi wa Chama.
Katika uchaguzi huo, Kaimu Mhariri wa Habari za Michezo wa gazeti la Mzalendo na Uhuru Wikiendi, Fred Majaliwa, alichaguliwa kuwa mwenyekiti kwa kuzoa kura 59 dhidi ya 28 alizopata Ignas Agustino ambaye alikuwa anatetea kiti hicho, huku Guruneti akipata kura tatu katika jumla ya kura 90 zilizopigwa.
Pia, wajumbe 37 wa Halmashauri Kuu walimchagua kwa kura 24 Emmanuel Ryoba Mkunyi kuwa katibu kata na kumwangusha Twaha Kisogo aliyepata kura 13, wakati Kapotele alirejea madarakani baada ya kuzoa kura 29 dhidi ya nane za Gaudencia Malongo.
Wajumbe waliochaguliwa kwenye Kamati ya Siasa ni Mayasa Subeya, Said Ndembo na Amos Chandala wanaoungana na wengine kwa nafasi zao katika chama na jumuia zake.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.