Habari za Punde

FCS YAENDELEZA MAFUNZO KWA ASASI ZINAZOPATA RUZUKU

 Meneja wa Kitengo cha Kujenga Uwezo wa Taasisi ya Foundation for Civil Society (FCS) Edna Chilimo, akiendesha mafunzo kwa washiriki kutoka Asasi za Kiraia kuhusu jinsi ya kutumia Ruzuku, wakati wa mafunzo hayo yanayoendelea hivi sasa katika Ukumbi wa Jengo la LAPF Makumbusho jijini Dar es Salaam. 
****************************
Na Ripota wa Mafoto Blog, Dar
Foundation for Civil Society (FCS) inaendesha mafunzo  kwa asasi zinazopata ruzuku ili kuzijengea uwezo asasi hizo kutekeleza miradi yao kwa ufanisi.
Mafunzo haya yanalenga kutazama changamoto zinazoyakabili mashirika katika utekelezaji wa miradi, masuala ya kuzingatia wakati wa kutekeleza miradi, aina ya wadau wanaohusika katika utekelezaji wa miradi, namna ya kubaini matokeo ya mradi pamoja na ukusanyaji visa vya mafanikio na suala zima la usimamizi na matumizi ya fedha.
Mafunzo haya yamefunguliwa na Mkurugenzi wa FCS Bw. Francis Kiwanga ambaye amebainisha nia ya FCS kuona sekta ya asasi za kiraia ikikua na akayataka mashirika yanayohudhuria mafunzo haya kuhakikisha kuwa yanakuwa na mbinu mbadala ya kutumia mafunzo haya hasa baada ya kumaliza mafunzo haya.
Akizungumza katika mafunzo hayo Meneja Ujenzi wa Uwezo kwa Azaki kutoka FCS Edna Chilimo alifafanua kuwa, FCS inatambua changamoto zinazoyakabili mashirika mbalimbali hali ambayo inasababisha kutofanikisha azma za kutekeleza miradi.
“Katika eneo letu la ujenzi uwezo wa mashirika tunaangalia kuwa mashirika yenu yanapaswa kuandika maandiko bora ya miradi. Ili mfanye hivi mnahitaji kujengewa uwezo. Pia tunaangalia eneo la kuwajengea uwezo wa Kujitegemea, uwezo wa kujiendesha yaani kutekeleza miradi na uwezo wa kushirikiana na mashirika mengine,” alisema Bi. Chilimo.
Mafunzo haya ya siku tatu yanafanyika jijini Dar es Salaam na mashirika mbalimbali yanashiriki kutoka maeneo tofauti nchini. FCS imekuwa ikifanya mafunzo ya aina hii kwa lengo la kuongezea uwezo sekta ya asasi za kiraia ili kuboresha utendaji wa mashirika mbalimbali yaliyopo nchini ili yaweze kufanikiwa katika kazi mbalimbali wanazozifanya. 
 Mwezeshaji akitoa mada 
Washiriki wakifuatilia mafunzo hayo kwa umakini.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.