Habari za Punde

KASI YA SIMBA YAPIGWA 'STOP' NA AZAM WAKITOKA SARE CHAMZI

Na Ripota wa Mafoto Blog, Dar
TIMU ya Azam Fc leo, imeshindwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani, baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Simba SC katika mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo, Simba SC imefikisha pointi nne sawa na Azam, huku ikiendelea kuongoza Ligi Kuu kwa wastani wa mabao, baada ya Prisons nayo kulazimishwa sare ya 2-2 na Maji Maji ya Songea leo Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Simba waliuanza mchezo huo kwa kasi na kiu ya kusaka bao la mapema na katika dakika ya nne tu, mshambuliaji Nicholas Gyan alikaribia kufunga baada ya mpira aliopiga kwa kichwa akiunganisha pasi ya kiungo Muzamil Yassin kuokolewa na kipa wa Azam, Mghana mwenzake, Razack Abalora.
Kipa wa Simba SC, Aishi Manula aliokoa mashuti mawili mfululizo ya nyota wa Azam kutoka Ghana, kwanza Enock Atta Agyei dakika ya 18 na baadaye Yahya Mohammed dakika ya 32.
Simba wakajibu mashambulizi hayo dakika ya 37 kupitia kwa kiungo wake kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima ambaye naye shuti lake liliokolewa na kipa Mghana wa Azam, Razack Abalora.
Kipindi cha pili, Azam FC wakakianza kwa kasi na kiu ya kusaka mabao na dakika ya 55 Yahya Mohammed akapiga nje akiwa kwenye nafasi nzuri kabla ya Simba kujibu dakika ya 56, baada ya mshambuliaji wake, John Raphael Bocco kubinuka vizuri tik-tak akijarbu kumalizia krosi ya kiungo wa Muzamil Yassin, lakini kipa wa Azam, Abalora akaokoa.
Kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ akapiga nje dakika ya 64 kabla ya kiungo wa Simba, Said Ndemla aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Shiza Kichuya aliyeumia kupiga juu ya lango dakika ya 70.
Refa Ludovic Charles akamuonyesha kadi ya njano beki Mzimbabwe wa Azam anayeweza kucheza kama kiungo pia Bruce Kangwa dakika ya 72 kwa ubishi. Refa huyo wa Mwanza akawaonyesha kadi za njano pia viungo Mcameroon wa Azam, Stephan Kingue dakika ya 78 na Mghana James Kotei wa Simba kwa kuchezeana rafu.
Sure Boy tena dakika ya 87 akaikosesha Azam bao baada ya kupiga nje kufuatia pasi nzuri ya Yahya Mohammed. Dakika ya 89, beki Salim Mbonde akaonyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea rafu Yahya Mohammed.
Kwa ujumla timu timu zote zilishambuliana kwa zamu, ingawa kucheza kwa kukamiana kunaweza kuwa kulichangia matokeo ya sare, kwani muda mwingi zilitumika nguvu kuliko maarifa. 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.