Habari za Punde

MAMLAKA YA USIMAMIZI WA BANDARI TPA YAKAMATA BOTI ILIYOTUMIKA KUIBA MAFUTA BAHARINI


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiangalia baadhi ya vifaa ikiwemo injini ya Boti, vilivyokamatwa mwishoni mwa wiki baada ya wahalifu kukurupushwa na kujitosa Baharini wakati wakijaribu kuiba mafuta kwa kutoboa bomba la Mafuta Baharini.
Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam 
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, ameiomba Serikali kuipatia Mamlaka yake vitendeakazi muhimu ili kukabiliana na vitendo vya uharamia wa bomba la mafuta katika bahari ya Hindi. 
Mhandisi Kakoko ametoa maombi hayo kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, aliyetembelea bandari hiyo upande wa mafuta na kuelezwa kuhusu tukio lililotokea juzi ambapo TPA wamekamata boti moja lilikuwa likitumiwa na wahalifu kuiba mafuta kutoka kwenye bomba, baharini. 
Katika tukio hilo watu wasio fahamika, wakiwa na mabomu na baadhi ya vilipuzi, walilitelekeza boti lao na kutoweka kusikojulikana kwa kupigambizi baharini baada ya walinzi wa doria kuwakurupusha kwa kurusha risasi hewani.
“Tunaomba tupatiwe vitendeakazi kwa ajili ya kikosi chetu kinachofanyakazi kubwa ya kupambana na uhalifu mbalimbali bandarini hasa magari ili kukiwezesha kikosi hicho kufanyakazi yake kwa ufanisi” alieleza Bw. Kakoko
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameahidi kuipatia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari vitendeakazi ambavyo viko ndani ya uwezo wake kama Waziri ili kuongeza udhibiti wa eneo la maji ya bahari lenye bomba la mafuta. 
“Ninawapongenza sana kwa kufanikisha kuwadhibiti maharamia hao ambao wamekuwa wakitumika kuharibu miundombinu ya bomba na mafuta na kuharibu mita za kupimia mafuta, nawaahidi kuwatimizia maombi yenu ya vifaa ambavyo viko ndani ya uwezo wangu” alisema Dkt Mpango’
Alisema kuwa vitendo vinavyofanywa na wahalifu hao vinakwamisha juhudi za Serikali za kuimarisha miundombinu yake na kusabisha hasara kwa wenye mafuta na kuikosesha Serikali mapato kutokana na vitendo hivyo vya kutoboa bomba na kuiba mafuta. 
Mbali na kushuhudia boti lililokamatwa pamoja na vifaa vyake ikiwemo injini na magaloni ya mafuta, Dkt, Mpango alipewa maelezo kuhusu mchakato unaoendelea wa kufunga mita mpya za kupimia mafuta (flow meters).
 Mhandisi Kakoko ameeleza kuwa mchakato unaendelea vizuri na kwamba huenda ukakamilika mapema mwakani hatua itakayosaidia kuongeza mapato ya Serikali bandarini hapo.
 Boti Jeupe lililonaswa na kikosi maalumu cha kuzuia uhalifu cha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) juzi wakati wahalifu wakijiandaa kutoboa bomba na kuiba mafuta kwenye kina kirefu cha Bahari ya Hindi. Wahalifu walifanikiwa kutokomea kusikojulikana baada ya kujitosa baharini, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.