Habari za Punde

MANJI 'AGOMEA' KUVULIWA UDIWANI KATA YA MBAGALA KUU
Na Mwandishi Wetu, Dar
MFANYABIASHARA maarufu nchini, Yusuf Manji mapema leo amesema kuwa hatambui kuvuliwa kwake udiwani wa Kata ya Mbagala Kuu na kwamba yeye bado ni diwani.
Manji ameyasema hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
wakati kesi ya yake uhujumu uchumi inayomkabili yeye na wenzake watatu ilipokuja kutajwa.
Kabla ya kusema hayo, wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi ameieleza mahakama kuwa upelelezi katika kesi hiyo, bado haujakamilika.
Akielezea kuhusu udiwani, Manji aliongeza kuwa, aliona habari kupitia gazeti la Mwananchi kwamba amevuliwa udiwani ila hajui kama ni kweli au la.
Amedai, mahakama imuagize Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), awaambie Halmashauri ya Wilaya ya Temeke kwamba walimkamata na sababu za kutohudhuria vikao kwa miezi miwili ni kwa kuwa hana dhamana.
Amesema, yeye amechaguliwa na wananchi na kwamba kama wanataka aende kwenye vikao, DPP aombe hati ya kumtoa gerezani ili akaudhurie vikao au wamuandikie barua yenye ajenda na kumbukumbu za vikao ili ajibu akiwa gerezani.
Ameongeza kuwa, ametumia zaidi ya milioni 70 za kwake binafsi na sio za halmashauri kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake na alikuwa anahudhuria vikao kabla hajakamatwa kwa kesi hizo nzito.
“Kwa kuwa naheshimu mahakama na ukubwa wa kesi hii sikuomba dhamana," amedai Manji. 

Mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji Mwenye Shati Nyeupe akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo.
************************************
Akijibu hoja hiyo, Hakimu Shaidi amewataka upande wa mashitaka kufuatilia suala hilo na kumueleza mshtakiwa kuwa maombi yake yamechukuliwa.
Wiki iliyopita Meya wa Temeke, Abdallah Chaurembo alitangaza kumvua udiwani Manji kwa kutohudhuria vikao.
Mbali na Manji.
Manji anashtakiwa pamoja na Meneja Rasilimali watu wa Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda, Mtunza stoo, Abdallah Sangey na Thobias Fwere.
Awali, Wakili wa washitakiwa, Seni Malimi aliiomba mahakama kutoa ahirisho fupi kwa washtakiwa kwa kuwa wanamaombi maalumu.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 18, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Manji na wenzake wanakabiliwa na tuhuma za uhujumu uchumi ambapo wanadaiwa kukutwa na vifaa mbali mbali za jeshi la polisi zikiwemo sare.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.