Habari za Punde

MHASIBU MKUU WA WILAYA SIKONGE MATATANI KWA KUKALIA JARADA LA MTUMISHI TOKA MWEZI JULAI MWAKA HUU.


 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (katikati) akitoa maelekezo  kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge juu ya utatuzi wa kero na hoja mbalimbali ambazo wananchi wameziwasilisha kwake jana wakati wa mkutano na wanachi. Wengine  ni Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Peres Magiri(kushoto) na Katibu Tawala Wilaya hiyo Renatus Mahimbali(kulia)
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Sikonge waliofika kuwasilisha kero zao wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akitoa maelekezo mbalimbali kwa wananchi hao na watendaji wa Wilaya hiyo . Zoezi hilo lilifanyika jana mjini Sikonge na wananchi 150.
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akihakiki upana wa barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami mjini Sikonge wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku mbili wilayani humo kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akitoa maelekezo jana mjini Sikonge kwa msimamizi wa barabara yenye urefu wa kilometa moja inayojengwa kwa kiwango cha lami katika eneo la Sikonge mjini kabla ya kutoa uamuzi wa kusitisha malipo kwa sababu kuonekana kujengwa chini ya kiwango. Picha na Tiganya Vincent-RS Tabora
***************************************
Na Tiganya Vincent, Sikonge
MHASIBU Mkuu (DT) wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge ameshitakiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa kukalia nyaraka za mstaafu kwa muda miezi zaidi ya miwili bila kushughulikia madai ya mtumishi huyo ya kulipwa kiunua mgongo.
Hali hiyo imetokea jana mjini Sikonge baada aliyekuwa Afisa Muuguzi Mkuu Paulo Madebe kudai kuwa tangu kumalizika kwa mkataba wake mwaka 2012 hadi leo hajalipwa kiinua mgongo chake licha ya taratibu mbalimbali kukamilika.
Madebe alisema kuwa alistaafu mwaka 2007 na baadaye alipata mkataba wa kuanzia mwaka  2010 hadi 2012.
Alisema kuwa baada ya kumalizika kwa mkataba wake amekuwa akifutilia fedha za kiinua mgongo na makato aliyokatwa kimakosa ya Mfuko wa PSPF bila mafanikio.
Madebe aliongeza kuwa baada ya kuona kuna ucheleweshaji kwa madai ya kukosekana kwa baadhi ya vielelezo aliamua kilifuatilia na kufanikiwa kuleta nyaraka katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge lakini wameshindwa kumalizia malipo yake.
Alisema kuwa pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kupitia madai na kutoa ushauri lakini DT amekataa kushighulikia Jarada lake ambapo aliongeza kuwa toka mwezi Julai liko mezani kwake.
Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amewapa siku mbili Mhasibu Mkuu wa Wilaya na Afisa Utumishi kuhakikisha jarida la mstaafu huyo linashughulikiwa na mhusika anajulisha ni lini atapata haki yake.
Alisema kuwa haiwezekani kila siku mzee kama yule anafutilia suala lake kwa zaidi ya miaka minne bila kupewa  ufumbuzi na hivyo kujikuta akipoteza muda na fedha zake badala ya kupumzika.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Peres Magiri alishauri kuwa ipoa haja ya kuendesha zoezi la uhamisho wa ndani kwa watumishi wa Halmashauri ya Sikonge kwa kuwa wengi wao wamekaa eneo kwa muda mrefu na kujenga mazoea ambayo yamefanya kushindwa kuwajibika ipasavyo.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora baada ya kumaliza zoezi la kusikiliza kero za wakazi wa Sikonge anatarajia kuendelea na Wilaya nyingine.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.