Habari za Punde

'MUHENGA' OKWI AENDELEA KUIBEBA SIMBA WAKIILAZA MWADUI 3-0

Na Devotha Kihwelu, Dar
MSHAMBULIAJI Mkongwem Emmanuel Okwi, leo tena ameendelea kuonyesha ukongwe wake na uzoefu wa ligi ya Bongo kwa kuendelea kuifungia Simba mabao ya kutosha baada ya leo kutupia tena mabao mawili kati ya matatu dhidi ya Mwadui Fc katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Mabao hayo yanamfanya raia huyo wa Uganda kufikisha mabao sita baada ya kucheza mechi mbili na kuwa kinara wa ufungaji katika msimamo hadi sasa.
Okwi alifunga mabao hayo katika kila kipindi ambapo la kwanza alifunga dakika ya saba wakati la pili akifunga dakika ya 57 kwa shuti kali la kushoto lililomshinda mlinda mlango Arnold Masawe.
Simba waliendelea kuliandama lango la Mwadui ambapo dakika ya 26 walifanya shambulizi kali na shuti la Shiza Kichuya likigonga mwamba na kutoka nje, huku bao la tatu na kufunga pazia la mabao katika mchezo wa leo likifungwa na John Bocco.
Akizungumza baada ya mchezo huo Kocha msaidizi wa Simba Jackson Mayanja, amesema kuwa uzoefu wa wachezaji wao ni sababu ya kupata ushindi wa magoli mengi kayika kila mchezo.
Mayanja amesema wana hakika mechi zinazofuata watazidi kufanya vizuri zaidi hususani katika kufanya mabadiliko ya wachezaji. 
Kutokana na mechi ya leo Simba inakuwa nafasi ya pili kwa alama 7 sawa na Azam huku Mtibwa Sugar ikiwa nafasi ya kwanza kwa alama 9.
Kwa upande wa kocha wa Mwadui Jumanne Ntambi alisema kwa upande wao wamepokea matokeo hayo na kufungwa kwao leo imewapa changamoto ya kwenda kufanya marekebisho kwa wachezaji wao.
Amesema wachezaji wake walicheza vizuri kwenye kipindi cha kwanza na hivyo kujipa matumaini kufanya vyema kwenye michezo mingine.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.