Habari za Punde

TANZANIA YAPOROMOKA VIWANGO VYA FIFA


SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA) limepanga orodha ya viwango vya timu bora za Taifa ambapo timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' imejikuta ikiporomoka kwa nafasi tano.
Mwezi uliopita Taifa Stars ilikuwa ikishika nafasi ya 120 ambapo katika viwango vilivyopangwa jana nchini Uswiss, Tanzania imeshika nafasi ya 125 katika nchi 206 duniani ambazo ni wanachama wa FIFA.
Tanzania ambayo imeshika nafasi hiyo imepitwa na nchi za Rwanda, Kenya na Uganda ambazo zimekuwa zikifanya vyema katika medani ya soka la ushindani kwa sasa duniani.
Katika sababu ambazo zimeonekana kuishusha Tanzania kwenye viwango hivyo ni kutolewa katika mechi ya mtoano ya kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CAN) inayofanyika mwakani nchini Kenya.
Katika viwango hivyo vya dunia, Ujerumani imeongoza ikifuatiwa na Brazil, Ureno, Argentina, Ubelgiji, Poland, Uswiss, Chile na Colombia ambapo nchi za Bahamas, Eritrea, Gibraltar, Somalia na Tonga zimeburuta mkia.
Barani Afrika nchi ya Misri imeongoza orodha ya viwango hivyo baada ya mafanikio ya muda mfupi tangu ilipokuwa ikifanya vibaya ambapo imefuatwa na Tunisia, Senegal, Congo, Nigeria, Cameroon, Burkina Faso, Ghana, Côte d'Ivoire na Morocco.
Viwango vya FIFA katika ngazi ya timu za Taifa vinaangalia uwezo wa mataifa katia mechi zake za mashindano na kirafiki ambazo zinatambulika na shirikisho hilo. FIFA inatarajia kupanga tena orodha ya viwango Oktoba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.