Habari za Punde

USAMBAZAJI DAWA MSD KATIKA VITUO VYA HUDUMA WILAYANI KILOSA WAFIKIA ASILIMIA 95

 Gari lenye namba za usajili SU 36435 la Bohari ya Dawa MSD, likiwalimekwama katika njia mbovu eneo la Kolosa mkoani Morogoro, wakati wakiwa katika harakati za kusambaza dawa katika Wilaya Kilosa mwishoni mwa wiki iliyopita.
******************************************
Na Mariam Mziwanda, Mororgoro
MKUU wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoi, amesema kwa sasa Wilaya hiyo inapata dawa na vifaa tiba kutoka Bohari ya dawa kwa asilimia 95.
Akizungumza na gazeti hili juzi Wilayani humo Mgoi alisema  maboresho ya huduma yanayotolewa na Bohari ya Dawa MSD Wilayani humo katika kuwafikishia dawa na vifaa tiba wananchi kwa wakati yanaridhisha.
Alisema wananchi wa Kilosa ni miongoni mwa watu waliokuwa wakiteseka kutokana huduma za afya.
Alisema hatua ya MSD kuboresha huduma zake kwa wakazi wa pembezoni ikiwemo kufikisha dawa na vifaa tiba moja kwa moja hadi vituoni imesababisha kupunguza kero katika sekta ya afya.
"Kiwango cha dawa kilichopo sasa ni asilimia 95 hivyo dawa zote muhimu zinapatikana na hatua ya MSD kufikisha dawa moja kwa moja vituoni imeleta unafuu wa huduma,"alisema.
Alisema kwa muda mrefu wilaya hiyo kumekuwa na changamoto  ya uhaba wa dawa na usimamizi mbovu katika udhibiti wa dawa ambapo kwa sasa ni historia.
"Katika kudhibiti upotevu wa dawa nimehakikisha kunaundwa  kamati maalumu yenye wajumbe watano ikiongozwa na Ofisa Tawala wa Wilaya kuangalia mapokezi na usambazaji wa dawa,"alisema.
Alisema hatua hiyo imeimarisha matumizi sahihi ya dawa katika vituo na kwenye mapungufu ya nyaraka ikiwemo kuorodhesha katika kitabu cha reja dawa zinazotoka.
Baadhi ya wafanyakazi wa MSD wakishusha dawa katika Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.
*****************************************
 Alisema kutokana na taarifa za tume hiyo ametoa onyo na kuagiza utunzaji sahihi wa dawa katika vituo vyenye upungufu.
Mgoi alisema kwa sasa changamoto aliyonayo ni elimu kwa wananchi ili kuelewa matibabu wanayotakiwa kupata katika Zahanati,Vituo vya Afya na Hospitali za Rufaa kwakuwa wengi wao wamekuwa wakilalamikia baadhi ya vipimo na dawa kutotolewa katika vituo vya huduma.
"Kama mtu ni mgonjwa wa kisukari au magonjwa mengine ambayo hawezi kupata matibabu yake katika zahanati ni lazima afuate utaratibu hivyo ni muhimu kuelewa zaidi,"alisema.
Naye Msimamizi wa Kituo cha Zahanati Kivungu Joyce Mhina alisema kituo hicho kinaagiza dawa kila robo mwaka  kutoka MSD na zinafika kwa wakati.
Alisema dawa ambazo zimekuwa na changamoto katika upatikanaji wake ni PPF na dawa za macho.
Alitoa wito kwa wanakijiji hao kuelewa kuwa ni vyema kufika hospitalini hapo wanapoumwa kwakuwa imekuwa ni kawaida wakiona gari la dawa wengi wao wanataka kupatiwa matibabu au dawa za malaria hata kama vipimo vinaonyesha wahana ugonjwa.
"Wanakijiji wakiona tu gari la MSD wanakimbilia kituoni na hata kama utampima na kubaini hana ugonjwa anataka umpe dawa ili tu akae nazo nyumbani kama akiba hali inayosababishwa na uelewa mdogo,"alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya usimamizi na upokeaji wa dawa kijijini hapo Christian Nchimbi alisema yeye na kamati yake wanaridhishwa na huduma zinazotolewa na MSD kwakuwa tatizo la dawa sasa ni historia.
Alisema zipo changamoto za majengo na uhaba wa watoa huduma lakini sio dawa na vifaa tiba hivyo serikali ione haja ya kumaliza tatizo hilo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.