Habari za Punde

VIINGILIO KUZIONA AZAM FC VS SIMBA JUMAMOSI NI 7000/=

KUZISHUHUDIA timu za Azam FC na Simba SC zikipepetana katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Jumamosi hii kiingilio ni shilingi 7,000 tu.
Timu zitakutana katika mchezo wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu huku kila kila timu ikiwa na pointi tatu mkononi baada ya kucheza mchezo mmoja kila moja.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, amesema kiingilio cha viti vya mzunguko kitakuwa ni sh 7,000 ambapo VIP itakuwa ni sh. 10,000.
Alisema wameamua kuweka kiingilio cha chini kwa ajili ya kuwapa fursa kwa mashabiki wenye hali ya chini pia kuweza kushuhudia mchezo huo.
Lucas alisema anaamini kiingilio hicho kitatoa nafasi kwa mashabiki wengi wa soka kujitokeza kwa wingi uwanjani siku hiyo ya jumamosi.
Ofisa huyo amewataka mashabiki wa timu hizo kujitokeza mapema uwanjani ili kuepuka usumbufu kutokana na udogo wa uwanja wa Azam Complex, ambao una uwezo wa kuchukua mashabiki 7000 pekee, ambapo alisema kuwa tiketi zitauzwa kulingana na uwezo wa uwanja huo na baada ya hapo tiketi hazitauzwa.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.