Habari za Punde

WADAU WAITAKA SERIKALI KUTEKELEZA SHERIA YA UPATIKANAJI WA TAARIFA

 Meneja Mradi wa Taasisi ya TWAWEZA, Annastazia Rugaba, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam, jana wakati akitoa Ripoti ya Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa iliyofanywa na Taasisi hiyo kwa nchi nzima.Picha na Muhidin Sufiani
*************************************
Duniani kote, sheria za upatikanaji wa taarifa zimebadilisha uhusiano uliopo kati ya wananchi na serikali. Wananchi wanapoelewa serikari yao inafanya nini, huweza kuchagiza maendeleo na wao wenyewe kunufaika. Wananchi wakiwa na taarifa za kutosha huweza kuchangia ipasavyo jitihada mbali mbali za maendeleo zenye kuleta maboresho ya jamii. Wakati mwingine, wanaweza kusaidia kufichua vitendo vya rushwa na uovu katika jamii zao. Mara nyingi upatikanaji wa taarifa huiwezesha serikali kuhakikisha mipango yake inaendana na hali halisi ya jamii. Pia taarifa huwasaidia watafiti kuchunguza zaidi na kutoa ufumbuzi wa matatizo sugu yanayozikabili jamii.  
Wananchi huweza kuuona umuhimu wao pale wanapoweza kufuatilia yale yanayoendelea katika jamii zao, na kuyachukulia hatua. Jamii bora ni ile inayoendesha shughuli zake kwa uwazi, ushirikishwaji na uwajibikaji; na yenye mifumo ya kuwapatia wananchi taarifa kwa uharaka. Jamii kama hiyo huwapa wananchi nafasi ya kushiriki kwenye masuala ya kijamii na huwapa nafasi za kutoa mawazo yao kwa uhuru, na demokrasia ya kuchagua viongozi wao na kuwawajibisha.
Sisi, wanachama wa umoja wa AZAKI zinazojishughulisha na masuala yahusuyo haki ya kupata taarifa, (Coalition on the Right to Information) tunaipongeza serikali kwa mara nyingine kwa kupitisha Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa (2016), hususani kwa kuthamini mawazo na maoni ya baadhi ya wadau kabla ya sheria hiyo haijapitishwa.
Hata hivyo, inasikitisha kuwa kanuni zinazoratibu utekelezaji sheria hii bado hazijaandaliwa, na pia kwamba sheria hii bado haijatangazwa rasmi katika gazeti la serikali. Sheria hii ilipitishwa mwaka mmoja uliopita lakini mpaka sasa bado haijaanza kutumika.
Katika kuelekea Siku ya Kimataifa ya Upatikanaji wa Taarifa (Septemba 28), tunaiomba serikali ianze hatua ya majadiliano ya kuandaa kanuni ili zikamilishwe mapema iwezekanavyo. Kwa sasa, tunaomba serikali itangaze sheria hii kwenye gazeti la serikali wakati mchakato wa kuaandaa kanuni unaendelea.
Kwa sasa, kuna uwezekano mkubwa kwamba wananchi hawapati taarifa pindi wanapozihitaji. Mwezi Januari/Februari mwaka 2016, watafiti, wakiwa kama wananchi wa kawaida, walitembelea ofisi 131 za serikali. Ofisi hizi zilikuwa katika wilaya 26 na takwimu zilizokusanywa zina uwakilishi wa kitaifa.
Meneja Mradi wa Taasisi ya TWAWEZA, Annastazia Rugaba, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam, jana wakati akitoa Ripoti ya Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa iliyofanywa na Taasisi hiyo kwa nchi nzima. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Umoja wa Haki ya kupata Taarifa  (CORI) Kajubi Mukajanga, Mshauri Mwandamizi wa Mawasiliano TWAWEZA, Risha Chande.
**************************************
Nia ya ziara hizi ilikuwa kutafuta taarifa fulani na watafiti hao walifanikiwa kupata taarifa za suala 1 kati ya masuala 3 (asilimia 33) waliyokuwa wanayahitaji. Hii inamaanisha kuwa, wananchi hawapati taarifa juu ya masuala mawili kati ya matatu wanayoyahitaji, kutoka katika ofisi za serikali. Japokuwa takwimu hizi zilikusanywa kabla ya kupitishwa kwa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa, hakuna sababu ya kudhani kuwa matokeo haya yamebadilika kwa kiwango kikubwa.
Kutokana na utafiti uliopita, tungependa kujikita kwenye maeneo yafuatayo: 
·         Asilimia 84 ya wananchi waliunga mkono mswada wa upatikanaji wa taarifa bungeni kabla haujapitishwa kuwa sheria, hii inaonesha kuwa wananchi wangependa kupata taarifa za serikali.
·         Asilimia 77 ya wananchi wanaamini kuwa wananchi wa kawaida wanapaswa kupata taarifa zinazomilikiwa na serikali.
·         Asilimia 80 ya wananchi wanaamini kuwa rushwa na matendo mengine maovu yatapungua iwapo wananchi watakuwa na uwezo wa kupata taarifa.
·         Asilimia 42 ya wananchi wangependa kupata taarifa zaidi zinazohusu sekta mbalimbali kutoka serikalini.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, anasema “Sote tunafahamu nguvu ya taarifa.  Upatikanaji wa taarifa ni muhimu sana na huwawezesha wananchi kujenga jamii ya kidemokrasia na yenye nguvu ambapo wananchi wanaweza kuzungumza kuhusu hatma ya maisha yao. Vyombo vya habari ni muhimu sana katika kuhakikisha suala hili linawezekana na serikali ina wajibu wa kuweka mifumo ya sheria na sera ili kufikia lengo hili.”
“Japokuwa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa, 2016 ilipitishwa mwaka uliopita” anaongeza, “hakuna kitu kikubwa kilichofanyika kuifanya sheria hiyo ianze kutumika na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa kwa uhuru kutoka serikalini. Ni wakati sasa wa sheria hii kuanza kutumika, hususani kwa kutengeneza kanuni muhimu kupitia njia ya mashauriano. Tofauti na hapo tunaweza kuhitimisha kwa kusema sheria hii ni kama danganya toto tu.” 
Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, anasema “Upatikanaji wa taarifa ni msingi imara katika ujenzi wa jamii ya kidemokrasia na yenye mafanikio endelevu. Kupitishwa kwa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa ni moja kati ya mambo yaliyoainishwa kuwa ya muhimu mwaka 2016 na Asasi za kiraia, vyombo vya habari na wananchi. Tunaiomba serikali ishirikiane na wadau katika kuandaa kanuni zinazoratibu utekelezaji wa sheria hii, na pia kutangaza rasmi matumizi ya sheria hii katika gazeti la serikali. Vilevile tunawakaribisha wananchi kuanza kuitumia sheria hii kujaribu kupata taarifa. 
Mkurugenzi wa Misa-TAN Gasirigwa Sengiyumva, anasema, “Njia pekee ambayo nchi inaweza kutarajia kuwa na wananchi wanaowajibika na wanaoshiriki vema katika mipango ya maendeleo ni kwa kuhakikisha wanapata taarifa. Wananchi wenye taarifa mara zote hufanya maamuzi yenye tija. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za binadamu, Dkt. Helen Kijo-Bisimba alihitimisha kwa kusema, “Kila Mtanzania ana haki ya kupata taarifa za serikali. Serikali wazi na inayowajibika lazima iwahakikishie wananchi wake uhuru wa kupata taarifa. Mwaka 2016 serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipitisha Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa lakini sheria hii imeacha mambo mengi yasiyo ya kawaida ambayo yanahatarisha haki ya kupata taarifa. Kwa mantiki hii tunaiomba serikali kupitia na kuanisha mambo hayo kuhusu Sheria ya Kupata Taarifa kabla sheria hiyo haijaanza kutumika. Baadhi ya mambo hayo ni muda wa kusubiri kabla maombi ya taarifa kujibiwa, wananchi wa Tanzania pekee kuruhusiwa kupata taarifa, wigo mdogo wa taarifa zinazopaswa kutangazwa, utata katika kuzuia baadhi ya taarifa, ada kwa ajili ya kupata taarifa na mambo mengine mengi yanahitajika kupitiwa.”

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.