Habari za Punde

YANGA KUIPA MAMILIONI SIMBA KATIKA SAKATA LA BUSWITA


SAKATA la mchezaji wa zamani wa Mbao FC, Pius Buswita kusaini mikataba na timu mbili za Simba na Yanga linaelekea ukingoni baada ya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuamuamuru kulipa kiasi cha fedha alichokichukua Simba ili aendelee kucheza.

Juni 15, mwaka huu Simba ilimsafirisha mchezaji huyo kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kuingia naye mkataba ambapo alisaini ‘mkataba mama’ wa klabu hiyo uliogharimu kiasi cha milioni 10.Siku moja baadae ilidaiwa kuwa mchezaji huyo alifuatwa na viongozi wa Yanga na kumshawishi kusaini mkataba nao baada ya klabu hiyo kufuata utaratibu na kanuni za usajili.
Yanga kabla ya kumfuata mchezaji huyo ilikwenda kufanya mazungumzo na viongozi wa Mbao FC ambao mchezaji huyo alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja ili kufuata utaratibu wa kumsajili.Kanuni za kuwasajili wachezaji zinasema kuwa klabu haiwezi kumsajili mchezaji mwenye mkataba na timu yake kabla ya kwenda kufanya mazungumzo na timu yake. 
Katika kipengele hiki Yanga ilionekana kufuata kanuni na taratibu za kumsajili mchezaji kabla ya kupeleka jina na mkataba wa awali TFF katika Kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji.
Baada ya Yanga kumtambulisha Buswita kuwa mchezaji wake na kujumuisha jina lake katika kikosi chao cha wachezaji waliowasajili msimu huu, Simba ilipeleka malalamiko TFF kwa ajili ya kudai kuwa mchezaji huyo aliwahadaa na kuwatapeli fedha zao ambazo walizilipa katika mkataba wa awali.
Katika kanuni za mkataba kipengele cha 69 cha mikataba ya wachezaji wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kinasema kuwa mchezaji wa kulipwa atakuwa huru pale mkataba wake na klabu yake utakapokuwa umekwisha. 
Mchezaji wa kulipwa ataruhusiwa kuingia mkataba na klabu nyingine iwapo mkataba na klabu yake utabakia chini ya miezi sita. Klabu inayotaka kuingia naye mkataba haina budi kuiarifu klabu yake ya sasa kwa maandishi kabla ya kufanya makubaliano yoyote ya mkataba na mchezaji huyo.
Kipengele cha (7) kinaeleza kuwa iwapo mchezaji wa kulipwa ataingia mkataba zaidi ya mmoja unaohusu kipindi kimoja cha usajili, masharti yaliyowekwa katika sura ya nne ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) yatatumika kutoa uamuzi.
Kipengele cha (6) kinatafsiri kuwa uhalali wa mkataba wa mchezaji hautakamilika/ hautahesabiwa hadi pale kuwe na matokeo mazuri ya upimaji wa afya, na kutolewa kwa kibali cha kufanya kazi (kwa wachezaji wa kigeni).
Katika kipengele cha (9) kinasisitiza kuwa mchezaji aliye na mkataba zaidi ya miezi sita hatoruhusiwa kujisajili na klabu nyingine kabla ya klabu yake mpya kuafikiana na ya zamani ambayo ina mkataba naye. Katika kipengele cha (11) kinabainisha kuwa usitishwaji wa mikataba ya wachezaji itafanywa kwa maandishi ili kamati kujiridhisha.Agosti 23, mwaka huu baada ya kamati hiyo kujiridhisha na kanuni iliamua kumfungia mchezaji huyo kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kugundulika amesaini mikataba miwili ambapo siku kadhaa baadae waliamua kuketi na Simba na Yanga ili kulimaliza suala hilo.Katika kikao hicho kilichofanyika jana katika ofisi za TFF zilizopo Karume, Dar es Salaam iliamua kuwa mchezaji huyo alipe milioni 10 alizochukua katika klabu ya Simba pamoja na milioni 1, 500,000 alizotumia katika usafiri wa ndege na malazi.

Akizungumza Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji, Elias Mwanjala, amesema wamefikia uamuzi huo baada ya kuwapa nafasi viongozi wa pande hizo mbili kuelewana.

Alisema uongozi wa timu hizo umekubaliana kumalizana kwa Yanga kulipa kiasi hicho ambacho mchezaji huyo amekichukua kutoka kwa Simba.
Mwanjala alisema baada ya kulipa fedha hizo Buswita ataruhusiwa kuchezea timu yake ya Yanga katika msimu huu.
Alisema Simba ilifanya ubabaishaji katika kuingia mkataba na mchezaji huyo kwa kuwa ilifanya naye mazungumzo ikiwa mchezaji huyo ana mkataba wa mwaka mmoja na timu yake ya zamani ya Mbao FC ambapo ni kinyume cha kanuni za ligi.
“Simba ilifanya ubabaishaji katika mkataba wake, imeingia mkataba na mchezaji ambaye ana mkataba na timu yake ya zamani zaidi ya mwaka mzima. Katika kufanya suluhu tumewaacha waelewane,” alisema Mwanjala.Alisema kabla ya mchezaji huyo kuanza kucheza atapewa barua ya onyo kali ikiwemo Simba ambayo imefanya ubabaishaji katika kuingia mkataba na mchezaji huyo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.