Habari za Punde

SERIKALI KUWAVALIA NJUGA VIONGOZI WALIOGAWA MAENEO YA HIFADHI ZA RELI

 MKURUGENZI wa Kampuni ya TRL, Masanja Kadogosa, akizungumza waakati akielezea utendaji kazi wa Kampuni hiyo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Atashasta Nditiye (kushoto) aliyefanya ziara ya utambulisho katika Ofisi za TRL baada ya uteuzi wake. Kulia ni Kaimu Naibu Mkurugenzi TRL, Focus Sahani.
**************************************************
SERIKALI  imesema inawafuatilia  baadhi ya viongozi  waliotumia madaraka  yao vibaya kwa  kuwapatia wananchi  maeneo ya hifadhi za reli  huku wakijua ni kinyume cha sheria.
Pia  imetenga  sh.bilioni 14 kwa ajili ya kurudisha  njia ya  reli  ya Arusha hadi  Moshi kutokana na eneo hilo  kuonekana kuwepo  na wafanyabiashara  wengi.
 Tamko hilo  lilitolewa na  Naibu Waziri wa Uchukuzi kupitia Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta  Nditiye  jijini Dar es Salaam leo, wakati alipofanya ziara  ya  kutembelea bodi ya  Shirika  la  Usafiri wa Reli  nchini (TRL) kwa lengo  la  kujitambulisha  tokea   baada ya kuteuliwa na Rais  Dk. John  Magufuli  kuiongoza wizara hiyo.
 Alisema  viongozi hao  ni  lazima wafuatiliwe kwani   wamekuwa sababu ya kuwepo   kwa  changamoto nyingi  katika taasisi ya  usafiri wa reli nchini.
Mhandisi  Nditiye alisema   changamoto hizo zimetokana na baadhi ya  wajanya  kushirikiana na   wananchi kuweza kuvamia maeneo ya reli huku  wakitambua kuwa ni kinyume cha sheria.
“Kwa wafanyakazi waliofanya hivyo ni lazima tuwafuatilie kwani lazima  tujenge  utamaduni  kwa  wananchi wa  kuweza  kuheshimu  mali za serikali,”  alisema.
 Pia  kutokana  na hilo, Mhandisi   Nditiye aliwataka wananchi wote waliojenga  eneo lolote  la hifadhi  ya reli  kubomoa  mara moja ili kupisha  mradi wa  ujenzi na uboreshaji wa  reli  nchini.
Alifafanua kwa wananchi ambao  mradi wa  reli umegusa maeneo yao , Serikali  imeiomba Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi kufanya tathimini  kwa ajili ya kuwalipa. 
 Kwa upande mwingine, Mhandisi  Nditiye, aliwaasa  wafanyakazi wa TRL  kuhakikisha   wanafanya kazi kwa kusimamia  mpango wa maendeleo  na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“ Haitapendeza  kuona mtu  anaenda kinyume  na adhma  ya serikali  katika utekelezaji  wa majukumu kwani  hatua  kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” alisema.
Kwa upande mwingine  serikali imetenga  sh. bilioni 14 kwa ajili ya  kurudisha  njia ya  reli  ya Arusha hadi  Moshi kutokana na eneo hilo kuwepo  na wafanyabiashara  wengi.
Akitolea ufafanuzi  suala hilo, Mkurugenzi  Mtendaji wa TRL, Masanja  Kadogosa  alisema  njia hiyo inatarajiwa kurudishwa  Julai  mwaka 2018 ambapo kiasi cha  fedha kilichotengwa kitasaidia kutengeneza  madaraja  na vituo  vya  treni  hizo.
“ Tunafanya hivyo kwa  eneo  Arusha hadi Moshi kwani   limeonekana  kuwa   na biashara  nyingi, hivyo tunawaomba wananchi wakae mkao wa kula ili kuwezesha serikali  kupata mapato yanayostahili kupitia sekta ya usafiri,”alisema.

Hata hivyo alizitaja  baadhi  ya changamoto wanazokabiliwa nazo kuwa ni jinsi ya  upatikanaji wa vibali  vya wafanyakazi wa kigeni, Vitendea kazi  na  Ubovu  wa njia  nyingi za reli nchini. 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.