Habari za Punde

KOCHA MAYANGA KUJIPIMA NA MTIHANI WA KWANZA NOVEMBA 11

NOVEMBA 11, mwaka huu katika mji wa Porto Novo utakuwa mtihani wa kwanza wa kocha, Salum Mayanga na kikosi kizima cha timu ya Taifa 'Taifa Stars' katika mechi ya kirafiki dhidi ya Benin.
Mechi hiyo ambayo ipo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), itakuwa mtihani kwa Mayanga juu ya kupanda katika viwango vya ubora wa FIFA ambapo kwa sasa tumeporomoka na kujikuta nafasi ya 136.
Mayanga anakwenda kucheza mechi ya kwanza ya kirafiki ugenini iliyopo katika kalenda ya FIFA tangu alipochukua mikoba hiyo kwa aliyekuwa kocha wa Stars, Charles Mkwasa.
Hadi sasa kocha huyo hajafungwa hata mchezo mmoja katika mechi alizocheza nyumbani za kirafiki za FIFA tangu amekinoa kikosi hicho. Mayanga alianza kwa ushindi mnono wa 2-0 dhidi ya Botswana, Tanzania 2-1 Burundi, na sareb ya 1-1 dhidi ya Lesotho.
Pia, kocha huyo alikiongoza vyema kikosi chake kupata ushindi wa 2-0 dhidi ya Botswana na mchezo uliopita ambapo alipata sare ya 1-1 alipokutana na Malawi katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mayanga ataingia katika mtihani huo baada ya mechi zake zilizopita kucheza na timu 'vibonde', ambapo kwa sasa amekutana na kigingi kutoka Afrika Magharibi.
Benin ambayo inashika nafasi ya 18 Afrika na 79 katika viwango vya Dunia ina nyota wengi wanaocheza ligi mbalimbali barani Ulaya akiwemo Stephane Sesegnon anayekipiga Montpellier ya Ufaransa.
Kupata nafasi ya kucheza na Benini, ni bahati iliyoje kwa kuwa mara kadhaa timu zinazoshika nafasi za juu Afrika zimekataa kucheza na Tanzania katika mechi za kirafiki ikiwemo Uganda na Kenya kwa kuhofia kuporomoka.
Katika kuhakikisha anakwenda kupambania pointi tatu katika mchezo huo utakaotoa hatima ya kupanda kwenye viwango vya FIFA, Mayanga ameita kikosi cha wachezaji 24.
Katika kikosi hicho Mayanga amewarejesha Farid Mussa kutoka Tenerrife ya Hispania na Elias Maguli anayekipiga Uarabuni.
Akitaja kikosi hicho Dar es Salaam, Mayanga aliwajumuisha wachezaji Abdallah Hamisi anayekipiga Sony Sugar ya Kenya, Yohana Mkomomola, Dickson Job na Abdul Mohammed ambao wote wanacheza katika kikosi cha chini umri wa miaka 20.
Alisema ameamua kuwaongeza wachezaji watatu kutoka katika kikosi cha Ngorongoro Heroes ili kuwapa uzoefu wa mechi za kimataifa kwa kuwa anaamini watakuwa msaada katika siku za karibuni.
Alisema mchezo huo utakuwa njia ya kupanda katika viwango vya FIFA hivyo atahakikisha anatumia mbinu za aina tofauti katika ushambuliaji ili kupata ushindi katika mchezo huo.
Mayanga, alisema mchezo huo utampa taswira ya maandalizi yake ya michezo ya kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Uganda, Capeverde na Lesotho. 
Mayanga amewaita makipa Aishi Manula ( Simba), Peter Manyika ( Singida United), Ramadhan Kabwili ( Yanga ), walinzi ni Boniphace Maganga ( Mbao ), Kelvin Yondani, Gadiel Michael ( Yanga), Erasto Nyoni ( Simba) na Dickson Job ( Mtibwa Sugar).
Viungo ni Farid Musa ( Tenerife, Hispania ) Himid Mao (Azam FC), Mzamiru Yassin, Shiza Kichuya ( Simba) , Simon Msuva, (DH Jadida/ Morocco ), Ibrahim Ajib ( Yanga), Hamis Abdallah ( Sony Sugar/ Kenya ), Abdul Mohamed.
Nahodha Mbwana Samatta(Genk, Ubelgiji), Mbaraka Yusuph (Azam), Elias Maguli na Yohana Mkomola ndiye washambuliaji pekee walioitwa.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.