Habari za Punde

KUELEKEA MARUDIO YA UCHAGUZI MKUU KENYA YAGAWANYIKA, ODINGA AITISHA MAANDAMANO

Kiongozi wa Muungano wa National Super Alliance (Nasa), Raila Odinga ametangaza maandamano ya siku mbili kuanzia kesho.
Odinga akizungumza katika Kanisa Katoliki la St Peter’s Kiminini, Trans-Nzoia amesema maandamano ya kesho Jumanne Oktoba 24,2017 na Jumatano yanalenga kushinikiza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufanya mageuzi kabla ya kuandaa uchaguzi wa urais wa marudio.
“Jumanne kutakuwa na maandamano, Jumatano pia tutaandamana na Alhamisi hakuna uchaguzi,” alisema Odinga ambaye amesusia uchaguzi huo wa marudio wa Oktoba 26,2017.
Wiki iliyopita Odinga alisema angetoa mwelekeo halisi Oktoba 25,2017 kuhusu hatua ambayo wafuasi wake watachukua wakati wa uchaguzi huo.
Kiongozi huyo wa upinzani amesema maandamano ni haki ya kikatiba ya Wakenya hivyo waandamanaji hawapaswi kuadhibiwa kwa kupigwa risasi na polisi.
Raila amedai ana ushahidi wa kuonyesha kuwa uchaguzi wa Oktoba 26 umesheheni udanganyifu.
“Tuna ushahidi wa kuonyesha kuwa uchaguzi wa Alhamisi una dosari. Tayari magari ya polisi yanasafirisha karatasi za kura. Ukweli ni kwamba kiasi kikubwa cha kura zilichapishwa jijini Nairobi na wala si Dubai kama mnavyoelezwa,” alisema.
Alidai kuwa kujumuishwa kwa Cyrus Jirongo katika karatasi za kura ni ithibati kwamba karatasi za kura zilichapishwa nchini Kenya.
“ Jirongo alitangazwa na korti kuwa amefilisika, mbona IEBC ilimjumuisha katika karatasi ya kura? Walijumuisha wagombea wote wanane kwa sababu karatasi zilikuwa zimechapishwa na Jubilee jijini Nairobi,” alisisitiza Odinga.
Alisisitiza kuwa hatashiriki uchaguzi wa Alhamisi ambao utawahusisha Rais Uhuru Kenyatta, Mohamed Abduba Dida, Dk Ekuru Aukot, Cyrus Jirongo, Dk Japhet Kaluyu, Profesa Michael Wainaina na Joseph Nyagah.
“Uhuru hana mshindani, anashindana peke yake. Sisi tunahitaji uchaguzi ambao Uhuru anashindana na Raila bali si uchaguzi wa mtu mmoja,” alisema.
 Waandamanaji wakirushiwa gesi ya kutoa machozi mjini Nairobi
******************************************
Badala ya uchaguzi huo mpya kutuliza hali nchini Kenya, unaonekana kuleta hali ya taharuki. Odinga, kiongozi wa muungano wa Nasa ameitisha maandamano siku hiyo ya uchaguzi baada ya mapema mwezi huu kutangaza hatashiriki katika uchaguzi huo kwasababu matakwa yake ya kuwepo mageuzi katika tume ya uchaguzi hayakutimizwa.
Kwa upande wake, Rais Uhuru Kenyatta ambaye aliuita uamuzi wa mahakama wa kuufutilia mbali uchaguzi wa rais wa Agosti nane kuwa ni 'mapinduzi', ameapa kushiriki katika uchaguzi wa Alhamisi hata kama mpinzani wake hatashiriki, hatua ambayo wachambuzi wanasema itaufanya uchaguzi huo mpya kutotambulika kisheria.
Jared Jeffrey mchambuzi wa shirika la kutoa ushauri wa kiuchumi barani Afrika NKC anaashiria kuwa Kenya huenda ikatumbukia katika ghasia iwapo uchaguzi huo utaendelea akiongeza kuwa upande wa Odinga huenda ukaanzisha wimbi jipya la maandamano zaidi.
Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zimetoa wito wa kuwepo amani nchini Kenya huku hali ya wasiwasi nchini humo ikizidi kabla ya uchaguzi wa Alhamisi wiki hii.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat wamesema pande mbili za kisiasa Kenya zinapaswa kujizuia dhidi ya kuchochea ghasia na kuvitaka vikosi vya usalama vya Kenya pia kujizuia dhidi ya kutumia nguvu kupita kiasi.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis pia ametoa wito wa kuwepo mazungumzo ya tija Kenya ambako anasema anafuatilia kwa karibu yanayojiri nchini humo na kuongeza analiombea taifa la Kenya liweze kukabiliana na changamoto linalozikabili katika mazingira ya majadiliano ya tija yaliyo na lengo la kufikia mazuri.
Wito wa amani watolewa kabla ya uchaguzi
Akiliongoza taifa katika maombi kwa ajili ya amani hapo jana, Rais Uhuru Kenyatta amewaomba wakenya kudumisha amani kabla ya uchaguzi wa Alhamisi.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga
*****************************************************
Wakati huo huo, Waendesha mashitaka watamshitaki dada yake Odinga, Ruth Odinga, seneta wa kaunti ya Kisumu Fred Outa pamoja na watu wengine kwa kuchochea ghasia baada ya maafisa wa tume ya uchaguzi kushambuliwa wiki iliyopita mjini Kisumu. Mashitaka mengine dhidi yao ni uharibifu wa mali, kuwazuia maafisa wa uchaguzi kuendesha shughuli zao na kukivamia kituo cha tume hiyo.
Maandamano ya karibu kila siku wakati mwingine yakiwa ya vurugu, cheche za maneno kutoka kwa wanasiasa na hali ya sintofahamu iliyoko Kenya kabla ya uchaguzi mpya wa rais unaotarajiwa Alhamisi wiki hii umeiweka nchi hiyo katika hali ya mashaka na kugawika.
Maandamano ya umma yamekuwa tukio la karibu kila siku tangu uchaguzi mkuu wa rais uliofanyika Agosti nane kufutiliwa mbali na mahakama ya juu. Uchaguzi huo ulikuwa umempa ushindi Rais Uhuru Kenyatta dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga.
Uhasama ulioongezeka unatia wasiwasi
Waandamanaji wamekuwa wakirushiwa gesi ya kutoa machozi, wanasiasa wa upinzani kukamatwa na wiki iliyopita kamishna mmoja wa tume ya uchaguzi IEBC Roselyn Akombe alitorokea Marekani akihofia maisha yake na kudai kuwa hakuna vile uchaguzi wa Oktoba 26 utakuwa wa huru na wa haki.
Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp/dpa 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.