Habari za Punde

LIGI YA WANAWAKE KUANZIA NOVEMBA 26

LIGI Kuu ya Wanawake Tanzania Bara inatarajiwa kuanza Novemba 26, 2017 katika vituo viwili vya Dar es Salaam na Arusha, imefahamika. 
Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Salum Madadi amesema Kundi A litakuwa Dar es Salaam na timu za Simba Queens ya jijini Dar Es Salaam iliyopanda daraja msimu huu.
Timu nyingine kwenye kundi hilo ni Mburahati Queens, JKT Queens, Evergreen zote za Dar es Salaam pamoja na timu za Fair Play ya Tanga na mabingwa watetezi - Mlandizi Queens.
Kundi B litakuwa na timu za Alliance ya Mwanza ambayo imepanda kutoka kituo cha Dodoma. Timu nyingine ni Marsh Academy pia ya Mwanza; Panama ya Iringa; Kigoma Sisterz ya Kigoma, Baobab ya Dodoma na Majengo Queens ya Singida. 
Time hizo zitapambana katika vituo hadi Desemba 9, mwaka huu kabla ya kutoa jumla ya timu nane kwa maana ya nne kutoka kila kundi. Timu hizo nane zitapambana katika hatua ya Nane Bora ya Ligi hiyo kuelekea ubingwa. Ligi inatarajiwa kumalizika Machi 28, mwakani. 
Kabla ya kuanza kwa ligi hiyo, TFF imetoa kalenda ya mashindano hayo ambako usajili utakuwa kati ya Oktoba 25 na Novemba 10, mwaka huu. 
Novemba 12 hadi 17, mwaka huu ni kipindi cha pingamizi  wakati Novemba 18, mwaka huu kutakuwa na kikao cha  Kamati ya Sheria kabla ya Novemba 20, mwaka huu kutoa leseni za wachezaji. 
Novemba 24, mwaka huu kutakuwa na Semina ya Viongozi wa klabu, Waamuzi na Makamishna jijini Dar es Salaam. 
Baada ya kumalizika hatua ya makundi Desemba 9, mwaka huu Ligi Kuu hatua ya Nane Bora ‘Super 8’ itaanza Desemba 20, mwaka huu.

KLINIKI YA SOKA LA WANAWAKE 
Kocha Mkuu wa timu ya mpira wa miguu ya Sweden, Pia Mariane Sundhage yuko nchini Tanzania na kesho Jumanne Oktoba 24, 2017 anatarajiwa kuwa na kliniki maalumu kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.
Kocha huyo mahiri ambaye mbali ya Sweden ambako anafundisha sasa, tayari alikwisha kuzinoa timu za taifa za  Marekani na China.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Salum Madadi, kliniki hiyo itaanza saa 3.30 asubuhi mpaka saa 6.00 mchana baada ya hapo kocha huyo atakuwa na nafasi ya kuzungumza na wanahabari.
“Karibu sana wanahabari kesho kushuhudia ufundi wa Kocha Pia Sundhage akizinoa baadhi ya timu ambazo TFF imezialika wakiwamo wachezaji wa timu ya taifa,” amesema Madadi alipokuwa anatambulisha ziara ya kocha huyo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.