Habari za Punde

MASIKINI TANZANIA DAIMAAAAAA, LATUPWA 'JELA' KWA SIKU 90

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
IDARA YA HABARI-MAELEZO 
Mtaa wa Samora, 
S.L.P 8031, 
DAR ES SALAAM. 
Simu: +255-22-2126826, 
Baruapepe:maelezo@habari.go.tz, 
Tovuti: www.tanzania.go.tz, 
Faksi: +255-22-2126834.  

TAARIFA KWA UMMA
SERIKALI YALIFUNGIA GAZETI LA TANZANIA DAIMA KWA SIKU 90
Dar es Salaam, Oktoba 24, 2017:
Serikali imesitisha uchapishaji na usambazaji wa gazeti la TANZANIA DAIMA kwa muda wa siku 90 (miezi mitatu) kuanzia leo. Agizo linahusu pia toleo la mtandaoni la gazeti hili. Uamuzi huu unatokana na makosa makubwa katika toleo na. 4706 la Oktoba 22, 2017 likiwa na habari ya uongo kuwa “Asilimia 67 ya Watanzania Wanatumia ARVs.”
Habari hiyo imeupotosha umma kwa kiasi kikubwa na kuleta taharuki huku ikikiuka kifungu cha 54(1) cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12, 2016.  Mhariri wa TANZANIA DAIMA alikiri kosa na kuomba radhi kwa upotoshaji uliofanywa katika habari hiyo.

Hata hivyo, pamoja na kuomba radhi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  ametumia mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari, baada ya jitihada na juhudi za muda mrefu za Serikali kuwashauri na kuwakumbusha wahariri wa gazeti hili kuhusu wajibu wa kufuata misingi ya taaluma na sheria. Miongoni mwa makosa ya hivi karibuni ni:
1.      Katika gazeti la Tanzania Daima toleo Na. 4381 la Desemba 2, 2016 ilichapishwa habari ya uzushi isemayo “Dangote Aivuruga Serikali.” Mwandishi wa habari hiyo aliandika uongo kumhusu Waziri wa Viwanda na Biashara na alishindwa kuthibitisha ukweli wa habari husika na gazeti likapewa KARIPIO KALI;

2.      Katika toleo Na. 4563 la Mei 31, 2017 ilichapishwa habari isemayo: “Mchanga Hofu Tupu” ikisheheni lugha ya kejeli na kashfa dhidi ya Serikali huku ikielezwa kuwa nukuu hizo zilitamkwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. George Masaju. Mhariri alikiri kuwa nukuu hizo zisizo na staha hazikuwa zimetamkwa na Mhe. Masaju. Mhariri akakiri kosa kupitia barua yenye Kumb. Na. FML 17/ADM/VOL.012/07 ya 31 Mei, 2017;

3.      Katika toleo  jingine Na. 4647 la Agosti 24, 2017 ilichapishwa habari isemayo: “Polisi Wasaka Bomberdier kwa Lissu.” Habari hii kwa kiasi kikubwa ilionyesha dharau, kejeli na kebehi kwa Serikali na Jeshi la Polisi ambao wana majukumu mazito ya kulinda usalama wa raia na mali zao lakini pia kuingilia uchunguzi wa kisheria. Mhariri alipotakiwa kuomba radhi, alitekeleza kwa muda na siku aliyoitaka, yaani Agosti 26, 2017 badala ya Agosti 25, 2017 aliyoelekezwa.

4.      Aidha, toleo Na. 4706 la tarehe 22 Oktoba, 2017 ilichapishwa habari yenye kichwa cha habari “Makinikia Pasua Kichwa-Bil. 700 Zazua Mijadala, Watu Wasema Kutoka Gari aina ya Noah  Hadi Bei ya Kinywaji.” Mhariri alionyesha kubeza na kuandika uongo wenye nia ya kuleta dharau dhidi ya hatua mbalimbali ambazo Serikali imefikia kuhusu makubaliano yaliyofikiwa kati yake na kampuni ya Barrick Gold Corporation. Katika barua ya Oktoba 22, 2017, Mhariri alijitetea kuwa aliandika tu maoni yaliyonukuliwa kutoka katika mitandao ya kijamii!

Habari hii ni ya uchochezi kwani hakuna ushahidi wa Serikali kuwahi kuahidi Noah, mazungumzo kuhusu fidia bado yanaendelea na zaidi gazeti hilo limeamua tu kukejeli vita ya kiuchumi inayoendeshwa na Serikali na kuzua uzushi kwa maslahi wanayoyajua wao.

Pamoja na gazeti lako kuomba radhi mara kwa mara na kurejea tena kwenye uandishi ule ule wenye utata, naona sasa uamuzi wa leo wa Serikali utasaidia kuifanya ofisi yako itafakari vizuri kuhusu mwelekeo wake na kujirekebisha kwa kuzingatia  misingi ya taaluma ya habari na Sheria za nchi,” inasema taarifa ya Waziri wa Habari kwenda kwa Mhariri wa TANZANIA DAIMA na taarifa hiyo inasisitiza zaidi:

Hata wakati huu ninapokuandikia barua hii, kwa kuzingatia ushauri wa wataalam wangu, gazeti lako la leo lina kichwa cha habari kinachomnukuu Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba Gavana Ndulu ametakiwa na Rais akabidhi ofisi haraka kwa mrithi wake wakati muda wake kwa mujibu wa Mhe. Rais unaisha miezi miwili baadae.” 
  
Serikali inaendelea kuwakumbusha wanatasnia ya habari nchini kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu na yenye wajibu, misingi na maadili, ndio maana Kanuni ya 1.7 (vii) ya kanuni za Maadili ya Wanataaluma ya Habari za Baraza la Habari (MCT) na kifungu cha kwanza cha Kanuni za Maadili za Chama cha Wanataaluma ya Habari Duniani (SPJ), vinasisitiza kuwa hakuna mbadala katika wajibu wa wanahabari kuandika ukweli na usahihi wa mambo.

Imetolewa na:
 Dkt. Hassan Abbasi
 Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali. 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.