Habari za Punde

UWT YATOA MSAADA KWA WATOTO YATIMA KUADHIMISHA SIKU YA UMOJA WA WANAWAKE

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania wa CCM Wilaya ya Kinondoni Anna Angaya kulia na Katibu Nuru Mwaibako kushoto wakimkabidhi Mwenyekiti wa kituo cha watoto yatima cha Maunga Center Zainabu Maunga baadhi ya zawadi walizozitoa Jumuiya hiyo katika kuadhimisha wiki ya UWT. Picha na Mariam Mziwanda
*******************************
Na Mariam Mziwanda
KATIKA kuadhimisha wiki ya Umoja wa Wanawake UWT Wilaya ya kinondoni imekabidhi msaada wa vifaa kwa ajili ya mahitaji mbalimbali kwa watoto yatima wa kituo cha Maunga Center kilichopo Ananasifu Kinondoni.
Akizungumza Mwenyekiti wa UWT Kinondoni Anna Angaya alisema Umoja huo umeona haja ya kuwafikia watoto yatima wa kituo hicho ili kupunguza changamoto zilizopo.
Alisema UWT inatambua kazi ya kulea watoto yatima ni ya kina mama hivyo ni wakati wa wanawake wote kuungana na kuhakikisha majukumu ya watoto hao yanawagusa kwa maslahi ya taifa.
“Machungu yote yana mama sisi ndio kina mama wa CCM hatuwezi kuwaacha watoto yatima ambao ni jukumu letu kuwaangalia, kuwasimamia na kuhakikisha wanakuwa wajenzi bora wa taifa hili,”alisema.
Anna alisema UWT inaamini msaada huo wa zaidi ya sh. Milioni moja utakuwa chachu kwa Jumuiya nyingine kumuunga Mkono Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Dk. John Magufuli katika kuwafikia wananchi wa chini.
Naye Mwenyekiti wa Kituo hicho Zainabu Maunga huku akiwa analia kwa huzuni alishukuru CCM kwa kuguswa na maisha ya watoto hao kwakuwa wapo katika mazingira magumu.
Alisema kituo hicho kwa sasa kina watoto yatima 48 ambao kati yao wapo wana wazazi mmoja mmoja na anasikitishwa na hatua ya ndugu wa watoto hao kuwatelekeza wanapowaleta kwakuwa bado watoto hao ni wadogo wanahitaji faraja ya familia.
“Napokea watoto hata wachanga badala ya watu kuwatupa ni bora waje waniwekee hapa nje nikiwakuta mimi namshukuru Mungu kwakuwa mimi mwenyewe sijazaa hivyo sina mtoto hii ni baraka kwangu lakini inapotokea pia ndugu au wazazi wa watoto wapo wasiwatelekeze kuja tu kuwasalimia kwao ni faraja hata kama hawana wazazi,”alisema.
Zainabu alisema kituo hicho bado kinakabiliwa na changamoto ya vifaa vya shule,shuka za kulalia,chakula mahali kwa ajili ya makazi kwakuwa sehemu waliyopo ni ndogo na imetolewa kama msaada.
Alieleza kuwa kituo hicho kimeanzishwa 2008 na kinaongozwa na lengo la elimu kwanza ili kuwafanya watoto hao kupata haki hiyo ya msingi katika mazingira yoyote waliyopo.
Alisema wanaamini CCM ni chama cha wanyonge na ndio maana kimekuwa mstari wa mbele kujali watoto yatima hivyo umadhubuti wake utaendelea kuwa imara katika kuongoza kila chaguzi. 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.