Habari za Punde

POINTI TISA TU KUMUONDOSHA AMA KUMBAKISHA LWANDAMINA YANGA

Na Ripota wa Mafoto Blog, Dar
KOCHA Mkuu wa Yanga, George Lwandamina huenda kibarua chake kikaota nyasi ikiwa atashindwa kuvuna pointi tisa katika michezo minne ijayo ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikiwemo dhidi ya Simba utakaopigwa Oktoba 24, mwaka huu.
Lwandamina ambaye ameanza vibaya katika mechi za ligi baada ya kutoka sare tatu katika mechi tano ilizocheza kikosi chake anatakiwa kuvuna zaidi ya pointi tisa katika mechi nne ili mashabiki na viongozi wa timu yake kuendelea kuwa na imani naye. 
Kocha huyo alianza kwa sare ya 1-1 dhidi ya Lipuli, ushindi wa 1-0 dhidi ya Njombe Mji, sare ya 1-1 dhidi ya Majimaji, ushindi wa 1-0 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara na sare tasa iliyopata wiki mbili zilizopita ilipocheza na Mtibwa Sugar katika dimba la Uhuru, Dar es Salaam.
Idadi hiyo ya mechi aliyocheza na matokeo aliyopata inawatia wasiwasi mashabiki wa timu hiyo ambapo msimu uliopita katika mechi tano za kwanza Yanga ilivuna pointi 13 katika mechi tano walizocheza. Yanga ilipata ushindi dhidi ya Yanga 3-0 African Lyon, sare tasa dhidi ya Ndanda, ushindi wa 3-0 dhidi ya Majimaji, waliibuka na ushindi wa 2-0 walipocheza na Mwadui FC na katika mechi ya tano waliichapa 1-0 Stand United ya Shinyanga.
Kikosi cha Lwandamina hadi sasa kimeshindwa kupata pointi tatu katika mechi zake mbili ilizocheza katika Uwanja wake wa nyumbani ambapo waliambulia sare mbili dhidi ya Lipuli na Mtibwa Sugar.
Kocha huyo anakabiliwa na kibarua kigumu cha mechi nne ngumu kabla ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kusimama kwa wiki mbili kupisha ratiba ya mechi za kimataifa za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Lwandamina anakabiliwa na kibarua hicho kufuatia michezo minne ambayo mitatu atacheza ugenini na mmoja nyumbani.
Huenda mechi nne zijazo za ligi zikatoa taswira ya hatima ya kocha huyo kutoka Zambia kutokana mwenendo wa kusuasua wa timu ya Yanga katika Ligi.
Kocha huyo ameendelea kukinoa kikosi chake kufuatia mechi yao ijayo dhidi ya Kagera Sugar itakayochezwa katika dimba la Kaitaba, Bukoba Jumamosi hii.
Lwandamina ambaye ameshaanza kuzomewa na baadhi ya mashabiki wa Yanga kufuatia kufanya vibaya kwa kikosi chake hatma yake inaweza kujulikana baada ya kucheza michezo hiyo minne ijayo.
Ikiwa kocha huyo atafanikiwa kuvuna zaidi ya pointi tisa katika michezo hiyo minne anaweza kuwatuliza mashabiki wa timu hiyo juu ya kumzomea akiwa uwanjani na kuhitaji aondoke lakini ikiwa tofauti na hivyo kuna uwezekano mkubwa kocha huyo kutemwa kukinoa kikosi hicho.
Ingawa kocha huyo aliisaidia Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita ana kibarua kigumu kuzizuia timu za Stand United, Simba na Singida United katika mechi zake nne zijazo kwa ajili ya kunusuru kibarua chake.
Baadhi ya wachezaji wazoefu wa zamani wa Yanga na makocha wameanza kuizungumzia hatima ya kocha huyo na sababu ya kufanya vibaya kwa Yanga katika mechi za kwanza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakongwe hao, kiungo wa zamani wa Yanga, Ally Mayay, alisema Lwandamina ana kazi kubwa ya kuhakikisha anafanya vyema na kikosi chake msimu huu kutokana na ushindani mkali uliopo katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu.
Alisema kikosi cha Lwandamina kinasumbuliwa na kuondokewa kwa wachezaji wazoefu akiwemo Haruna Niyonzima na Simon Msuva hivyo itachukua kipindi kirefu timu hiyo kufanya vyema.
Mkongwe huyo wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, alisema ikiwa Yanga inataka kufanya vyema, Lwandamina anatakiwa kubadili aina ya mfumo wa uchezaji anaoutumia kwa kuwa hana wachezaji wenye kasi ya kufanana na Msuva. 
Naye beki wa zamani wa timu hiyo, Bakari Malima 'Jembe ulaya', alisema kikosi hicho kitapata shida katika ligi msimu huu kwa kuwa Lwandamina hakufanya usajili wa maana kwa ajili ya kuifanya timu yake kuwa tishio.
Alisema wachezaji waliotimka katika kikosi hicho msimu uliopita wameathiri mfumo wake hivyo ni muhimu kuwabadilishia mfumo wachezaji vijana alionao ili kuendana na ligi.
Alisema Lwandamina kama anataka kupata matokeo mazuri katika mechi za ligi msimu huu anatakiwa kukifua upya kikosi chake hususani katika safu ya ushambuliaji ambayo wachezaji wake wamekosa umakini.
Kwa upande wa kocha msaidizi wa zamani wa timu hiyo, Kennedy Mwaisabula, alisema Yanga inasumbuliwa na ukosefu wa washambuliaji wazoefu ambao ni Donald Ngoma na Amis Tambwe ambapo kwa sasa wanauguza majeraha.
Alisema Yanga imezoea kucheza soka ya kutumia mipira mirefu na kasi hivyo kukosekana kwa wachezaji hao kunasababisha kikosi chao kutokuwa na makali.
Kocha huyo na mchezaji wa zamani wa Yanga, alisema Lwandamina anakazi ya kubadilisha mfumo ikiwa anataka kupata matokeo katika mechi nne zijazo kabla ya kusimama kwa ligi.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.