Habari za Punde

TEMEKE NA MBEYA ZAFANIKIWA KUTEKELEZA MPANGO WA MAREKEBISHO YA TABIA KWA WATOTO WALIOKINZANA NA SHERIA

Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinisa, Wazee na Watoto Bw. Darius Damas akielezea jambo kwa washiriki wa kikao cha mwaka cha Tathmini ya Utekelezaji wa Mpango wa Kijamii wa Marekebisho ya Tabia kwa watoto waliokinzana na Sheria kilichofanyika katika ukumbi wa NHIF Mjini Dodoma.
Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii Bw. Rabikira Mushi (katikati) akizungumza na wadau wa utekelezaji wa Mpango wa Kijamii wa Marekebisho ya Tabia kwa Watoto waliokinzana na Sheria alipokuwa akifungua kikao cha mwaka cha Tathmini ya Mpango huo katika ukumbi wa NHIF Mjini Dodoma.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto Bi Magreth Mussai akifafanua jambo wakati kikao cha Tathmini ya mwaka ya Mpango wa Kijamii wa Marekebisho ya Tabia kwa watoto waliokinzana na Sheria kilichojumuisha Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii, TAMISEMI, na wadau wa Watoto kilichofanyika katika ukumbi wa NHIF Mjini Dodoma.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Jiji la Mbeya Bi. Bupe Joel akielezea mafanikio ya utekelezaji wa Mpango wa Kijamii wa Marekebisho ya Tabia kwa watoto waliokinzana na Sheria katika Jiji la Mbeya wakati wa kikao cha mwaka cha tathmini ya mwaka ya Mpango huo kilichofanyika katika ukumbi wa NHIF Mjini Dodoma.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Temeke Bi. Neema Mambosho akielezea mafanikio ya utekelezaji wa Mpango wa Kijamii wa Marekebisho ya Tabia kwa watoto waliokinzana na Sheria katika Wilaya ya Temeke wakati wa kikao cha mwaka cha tathmini ya mwaka ya Mpango huo kilichofanyika katika ukumbi wa NHIF Mjini Dodoma.
Mkurugenzi wa Kituo cha Malezi ya Watoto Kigamboni(KCC) Bw.Nassor Mkwesu akielezea mafanikio ya utekelezaji wa Mpango wa Kijamii wa Marekebisho ya Tabia kwa watoto waliokinzana na Sheria katika Kituo cha Malezi ya watoto Kigamboni wakati wa kikao cha mwaka cha tathmini ya mwaka ya Mpango huo kilichofanyika katika ukumbi wa NHIF Mjini Dodoma.
Baadhi ya wadau wa Utekelezaji wa Mpango wa Kijamii wa Marekebisho ya Tabia kwa watoto waliokinzana na Sheria wakisikiliza mada na shuhuda mbalimbali za mafanikio ya Mpango huo wakati wa kikao cha mwaka cha tathmini ya utekelzaji wa Mpango huo kilichofanyika katika ukumbi wa NHIF Mjini Dodoma. 
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
**********************************************
Na Mwandishi Wetu- Dodoma
Halmashauri za Temeke na Mbeya zimeonesha mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Mpango wa Kijamii wa Marekebisho ya Tabia kwa Watoto waliokinzana na Sheria ambapo kwa miaka mitano kuanzia 2012 mpaka 2017 jumla ya watoto 1000 wamefikiwa na kupewa msaada wa kisheria na wengine kufutiwa mashtaka.
Takwimu hizi zimetolewa mjini Dodoma na Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii Bw. Rabikira Mushi alipokuwa akifungua kikao cha mwaka cha Tathmini ya Mwaka ya Mpango wa Kijamii wa Marekebisho ya Tabia kwa watoto waliokinzana na Sheria.
Bw. Rabikira Mushi ameongeza kuwa katika watoto 1000 waliofikiwa, watoto 416 walipelekwa katika vituo vya marekebisho ambapo wengine wamerudi shule, kuhitimu mafunzo ya VETA na kurejeshwa katika hali ya heshima na staha.
“Niseme Serikali itakuwa inaendelea kutekeleza Mpango huu kwa ubia baina ya Asasi za Kirai na Halmashauri husika” alisema Bw. Mushi. 
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii wa Jiji la Mbeya Bi. Bupe Joel amesema kuwa kwa mkoa wa Mbeya mpango huu ulianza kutekelezwa kuanzia Novemba, 2014 hadi Oktoba, 2017 kama mpango wa majaribio na umefanikiwa katika utekelezaji wake kwa kusaidia watoto 185.
“Mpango huu umesaidia sana kupunguza idadi ya kesi za jinai watoto katika Mahakama kwa Halmashauri ya Jiji la Mbeya” alisema Bi Bupe.
Aidha Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Temeke Bi. Neema Mambosho amesema kuwa Halmashauri ya Temeke kwa kushirikiana na vituo vya utekelezaji wa mpango imekuwa ikiangalia njia mbali mbali za kuwasaidia watoto mara tu wamalizapo muda wao wa kuwa katika mpango wa marekebisho ya tabia (after care plan). 
Ameongeza kuwa Katika kufanya hivyo Halmashauri imeweza kuwapatia nafasi ya mafunzo VETA watoto 14 pamoja na kuwasaidia watoto 53 ambao walishaacha shule kurudi shuleni. 
Madhumuni makubwa ya Mpango wa Marekebisho ya Tabia kwa Watoto waliokinzana na Sheria ni kuwachepusha watoto kuingia katika mfumo wa mahakama na kwenda magerezani kutoka na makosa mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.