Habari za Punde

TUMEJIFUNZA MENGI KUTOKA KWA MALAWI: SAMATTA

 NAHODHA wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' anayekipiga katika timu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji, Mbwana Samatta,  amesema mchezo dhidi ya Malawi umetoa darasa kwao.
Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' ililazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Malawi katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Samatta alisema wamejifunza kutodharau timu yeyote wanayokutana nayo.
Samatta alisema hawakuamini kama Malawi wangekuja tofauti na walivyofikiria.
Alisema walikuwa wakiamini kuwa wataifunga Malawi kwa njia rahisi kama ilivyofanya Afrika Kusini katika michuano ya COSAFA lakini ilikuwa tofauti na ujio wao wa sasa.
Alisema kikosi cha Malawi kilijiandaa vya kutosha jambo ambalo limewapa somo kutoidharau timu yoyote watakayokutana nayo.
Nahodha huyo alisema ni wakati wa wachezaji wa Taifa Stars kufikiria zaidi katika mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika itakayofanyika 2019 nchini Cameroon.
Alisema sare hiyo imewapa umuhimu wa kuzifikiria timu za Uganda, Lesotho na Cape Verde ambazo zipo katika kundi moja kwa ajili ya kuchuana.
"Kila timu imekuja tofauti kwa sasa, sikutegenea kama Malawi ingecheza hivi, imekuja tofauti na vile vilivyofikiria. Ni wakati wa kubadilika na kuongeza umakini," alisema Samatta.
Alisema matokeo dhidi ya Malawi yamewapa somo kuongeza juhudi na umakini wanapokuwa dimbani katika mechi zao zijazo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.