Habari za Punde

KOCHA NINJE AWEKA WAZI SIRI YA UTEUZI WA KIKOSI CHA KILIMANJARO STARS

Kocha Mkuu wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania Bara, ‘Kilimanjaro Stars’, Ammy Conrad Ninje, amesema kwamba ameteua kikosi hicho kwa kuzingatia mambo makuu matatu.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Ninje alitaja kikosi cha wachezaji 20 kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji mwaka huu wa 2017 ambako amesema: “Kwanza nataka mchezaji ambaye ana njaa ya mafanikio…
“…Sehemu pekee ya kupata mafanikio  ni pamoja na kucheza timu ya taifa. Pili, nataka wchezaji wanaofundishika na tatu nataka wachezaji wanaokubali kufundishika,” amesema Ninje.
Ninje - Kocha wa Daraja ‘A’ la Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), alitaja kikosi hicho Jumamosi Novemba 18, 2017 kwenye Ukumbi wa Hosteli za TFF, Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.
Kikosi hicho kinachotarajiwa kuingia kambini Jumapili Novemba 26, mwaka huu jijini Dar es Salaam kina makipa Aishi Manula (Simba SC) na Peter Manyika (Singida United).
Walinzi ni Gadiel Michael (Young Africans), Boniphace Maganga (Mbao FC), Kelvin Yondani (Young Africans), Kennedy Juma (Singida United), Erasto Nyoni (Simba SC) na Mohammed Hussein (Simba SC).
Viungo wa kati ni Himid Mao ambaye ni Nahodha (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Mzamiru Yassin (Simba SC), Raphael Daud (Young Africans), Shizza Kichuya (Simba SC), Abdul Hilal (Tusker/Kenya) na Ibrahim Ajib (Young Africans).
Washambuliaji ni Mbaraka Yussuph (Azam FC), Elias Maguri (Dhofar/Mascat, Oman), Daniel Lyanga (Fanja FC/Mascat) na Yohana Mkomola (Ngorongoro Heroes). 
Benchi la Ufundi linaundwa na yeye Ninje ambaye ni Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa). 
Katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Desemba 3, mwaka huu, Kilimanjaro Stars imepangwa Kundi ‘A’ pamoja wenyeji Kenya, Rwanda na Libya ambayo ni timu mwalikwa kutoka Kaskazini mwa Afrika.
Kilimanjaro Stars ambayo imewahi kutwaa mara tatu taji hilo la Chalenji tangu kuanzishwa kwake, itaaza kampeni za kurudisha heshima yake dhidi ya Libya katika kundi hilo la A utaofanyika Desemba 3, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.