Habari za Punde

MATANO YA YANGA YANAPENDEZA ZAIDI, UWANJA WA UHURU DAR DHIDI YA MBEYA CITY


Kiungo wa Yanga Pius Buswita (kusoto) akichuana kuwania mpira na beki wa Mbeya City, Sankani Mkandawile, ambapo katika hekaheka hii ilizaa bao la kwanza la Yanga, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, leo. Katikati yao ni kipa wa Mbeya City, Fikilini Bakari. 
Obrey Chirwa akitamba na mpira wake bada ya kutupia matatu katika mchezo huo.
******************************************************
*Chirwa apiga 'hat trick'
Na Ripota wa Mafoto Blog,Dar
MABAO matano ya Yanga dhidi ya Mbeya City katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam,jioni ya leo yametosha kipa ushindi mnono wa mabao wa kwanza tangu kuanza kwa Msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
Katika mchezo huo Yanga walionekana kufunguka zaidi na kucheza kwa maelekezo huku muda mwingi wakishambulia na kuibuka na ushindi huo.
Mashujaa wa chezo huo leo walikuwa ni Obrey Chirwa aliyetupia mabao matatu katika dakika ya 19, 50 na 59 na Emmanuel Martin mabao mawili katika dakika ya 82
Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 20 baada ya kushuka dimbani mara 10, huku Chirwa akifikisha mabao sita katika mbio za kufukuzia kiatu cha dhahabu.
Chirwa akikabidhiwa mpira wake na mwamuzi wa mchezo huo baada ya kutupia mabao matatu kati ya matano dhidi ya Mbeya City.
Hapa Yusuph Mhilu sijui alining'inizwa kidali ama vepe.....
***************************************
Yanga, tangu mapema ilionyesha uchu wa kufunga bao baada ya wachezaji wake kuwa wa kwanza kubisha hodi langoni mwa Mbeya City katika dakika ya tatu tu ya mchezo.
Mbeya City kupitia Frank Ikobela alitaka kuwashtua Yanga kwa kupiga mkwaju uliotoka nje katika lango la wapinzani wao dakika moja baada ya wenyeji kuanza kuwashambulia.
Kosa hilo la Mbeya City liliwafanya Yanga kuamka na kuliandama lango la wapinzani huku wakichezeshwa na viungo wao, Raphael Daud aliyewachambua mabeki pinzani na kufumua kiki ambayo ilidakwa na kipa Firikini Bakari kwenye dakika ya saba, ambapo dakika tano baadaye Eliud Ambokile alipiga shuti ambalo pia lilishia mikononi kwa Youthe Rostand.
Mpira wa adhabu iliyopigwa na Omary Ramadhani wa Mbeya City pia haikuweza kutinga wavuni katika mchezo huo ambao katika robo ya kwanza ya mchezo washambuliaji na viungo wa timu zote hawakucheza kwa utulivu.
Geofrey Mwashiuya akipiga krosi
Bao la tanoooooooo...................................
***********************************************
Ilichukua hadi dakika 19 Chirwa 'kuzindua' karamu ya mabao ya Yanga baada ya Pius Buswita kuudokoa mpira uliopita katikati ya beki na kipa wakati wakigombea huku wachezaji wa Mbeya City wakizani umetoka nje ya mstari.
Mkandawile alikuwa analinda mpira utoke nje ili uwekwe golikiki na kuweza kupigwa kuelekea lango la Yanga, lakini kibao kiligeuka kufuatia Chirwa kufunga na 'ngoma' kuwekwa kati.
Martin licha ya kufanya kazi nzuri ya kutengeneza bao la kwanza, alifunga la pili dakika ya 22 baada ya kumtoka kipa wa Mbeya City na kutupia mpira wavuni.
Chanzo cha kufungwa mabao hayo ni kutokana na viungo wa Yanga, Pato Ngonyani na Daud kuivuruga Mbeya City katika safu ya kiungo.
Beki wa Yanga, Gadiel Michael, akimtoka beki wa Mbeya City na kupiga krosi ya bao la ttano lililofungwa na Emmanuel Martin.
Juma Abdul na Hassan Mwasapili wangekuwa makini kila mmoja angeweza kufunga katika dakika ya 34 na 36, baada ya Chirwa kumpa pasi beki huyo lakini alipiga mpira kwa mguu wa kushoto ukatoka nje. Pia, Mwasapili alishindwa kuunganisha wavuni pasi ya Mohamed Samatta.
Dakika ya 50 Chirwa alifunga bao lake la pili na tatu kwa Yanga kupitia penalti iliyotolewa na mwamuzi Athuman Lazi, kufuatia kipa Fikirini kumfanyia madhambi Raphael Daud katika kisanduku cha hatari.
Kipa huyo wa Mbeya City pia alionyeshwa kadi ya njano kwa kosa hilo.
Kama hiyo haitoshi, Chirwa dakika tisa baadaye aliandika 'hat trick' kwa maana ya kufunga mabao matatu katika mchezo mmoja, kutokana na kupokea pasi ya kiufundi kutoka kwa Ibrahim Ajib na kufunga kiulaini.
Ajib alinyunyiza mpira katikati ya mabeki na kumpa pande Mzambia huyo ambaye hakufanya makosa kufunga bao hilo na kufikisha sita katika ligi kuu msimu huu.
Bao la tano ambalo lilitosha kuifanya Yanga ipendeze zaidi liliwekwa kwenye kamba na Martin dakika ya 82, huku mabingwa hao watetezi wakikosa bao la sita kutokana na Geoffrey Mwashuiya aliyechukua nafasi ya Chirwa dakika ya 75, akishindwa kufunga akiwa ana kwa ana na kipa wa Mbeya City.
Mashabiki wa Mbeya City wakilalama jambo....
Emmanuel Martin (wa tatu kulia) akiwania mpira na Babu Ally wa Mbeya City (kushoto) wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam
Wachezaji wa Yanga wakimpongeza Martin
Kipa wa Mbeya City,Fikirini Bakari akiokoa moja ya hatari langoni kwake.....
Buswita akijaribu kuwatoka mabeki wa Mbeya City
Mtoto alishuka kutoka jukwaa na kuomba kupiga picha na Ibrahim Ajib katika benchi la Yanga...
*********************************************
Kikosi cha Yanga: Youthe Rostand, Juma Abdul, Gadiel Michael, Vicent Andrew 'Dante', Nadir Haroub 'Cannavaro', Pato Ngonyani, Pius Buswita/ Juma Mahadhi, Raphael Daudi, Obrey Chirwa/ Yusuf Mhilu, Ibrahim Ajib/ Geoffrey Mwashiuya na Emmanuel Martin. 

Kikosi cha Mbeya City: Fikirini Bakari, Rajabu Isihaka, Hassan Mwasapili, Ally Lundenga/ Ramadhani Malima, Sankani Mkandawile, Babu Ally, Mrisho Ngassa/ Victor Hangaya, Mohamed Samatta, Omary Ramadhani, Frank Ikobela na Elliud Ambokile/ Idd Selemani.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.