Habari za Punde

TAASISI YA MOI YAWEKA WAZI MAFANIKIO YAKE, MIAKA MIWILI YA UONGOZI WA RAIS DKT. MAGUFULI

 Meneja Uhusiano toka Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI  Jumaa  Almasi (kulia) akielezea mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka miwili ya Utawala wa Rais John Pombe Magufuli mapema hii leo Jijini Dar es Salaam, (kushoto) ni Ofisa Uhusiano wa taasisi hiyo Patrick Mvungi.
 Meneja Uhusiano toka Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI)  Jumaa  Almasi (katikati) akielezea mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka miwili ya Utawala wa Rais John Pombe Magufuli mapema hii leo Jijini Dar es Salaam, kushoto ni Afisa Uhusiano wa taasisi hiyo Patrick Mvungi na kulia ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Fatma Salum.
Afisa Uhusiano toka Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI  Patrick Mvungi (kushoto) akielezea mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka miwili ya Utawala wa Rais John Pombe Magufuli mapema hii leo Jijini Dar es Salaam, katikati ni Meneja Uhusiano wa taasisi hiyo Jumaa  Almasi na kulia ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Fatma Salum. Picha na Eliphace Marwa - Maelezo
**********************************
Na Fatma Salum (MAELEZO)
Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) imenufaika na mabadiliko chanya yaliyofanyika ndani ya miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli.
Mabadiliko hayo yameboresha utoaji wa huduma kwa wagonjwa na mazingira bora kwa watoa huduma jambo ambalo limeleta faraja kwa wananchi wanaofika kwenye taasisi hiyo kupata huduma mbalimbali za tiba ya mifupa.
Hayo yameelezwa leo na Meneja Uhusiano wa MOI Jumaa Almasi  wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya taasisi hiyo kwenye miaka miwili ya uongozi wa Rais Magufuli.
“Maboresho yaliyofanyika katika kipindi hiki kifupi yameiwezesha MOI kutoa huduma bora kwa wakati ukilinganisha na miaka mingine iliyopita,”  alisema Almasi.
Akifafanua kuhusu maboresho hayo, Almasi alisema kuwa kwa sasa MOI kuna ongezeko la vitanda vya kulaza wagonjwa kutoka vitanda 159 hadi 340 hivyo hakuna tena changamoto ya wagonjwa kulala sakafuni.
Alieleza kuwa idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji imeongezeka hadi kufikia wagonjwa 700 kwa mwezi kutokana na Serikali kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba na nafasi ya kulaza wagonjwa.
Aidha alisema kuwa katika kipindi cha miaka miwili kuna ongezeko la wagonjwa wanaopata huduma za kibingwa MOI (Super Specialized Services) ambapo idadi kubwa ya wagonjwa wameweza kufanyiwa upasuaji mkubwa wa nyonga, mgongo, ubongo, upasuaji wa matundu, magoti, kiuno pamoja na upasuaji wa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Kwa upande mwingine Afisa Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi alieleza kuwa pamoja na upasuaji mkubwa uliofanyika katika kipindi hiki pia viungo bandia 1,362 vimetengenezwa kutokana na Serikali kurahisisha upatikanaji wa malighafi za kutengenezea viungo hivyo.
“Awali wagonjwa wengi walikuwa wakipelekwa nje ya nchi kwa gharama kubwa ili kuwekewa viungo vya bandia, lakini sasa wanaweza kupata huduma hiyo wakiwa hapa hapa nchini,” alisema Mvungi.
Mvungi alieleza kuwa Serikali imetoa shilingi bilioni 16.5 kwa ajili ya kukamilisha mradi wa MOI awamu ya tatu (MOI Phase III) ambapo zitatumika kununulia vifaa ikiwemo CT SCAN, MRI, mashine mbili za XRAY na Ultrasound ya kisasa.
Pia Serikali imekuwa ikiwajengea uwezo wataalamu wa hapa nchini kwa kuleta wataalamu wengine kutoka mataifa mbalimbali duniani ili waweze kujifunza na kubadilishana uzoefu.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.