Habari za Punde

CHUO KIKUU CHA SAUT NA MATAWI YAKE CHATOA WAHITIMU 8687

Dkt. Darius Mkiza akitunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika fani ya Mawasiliano ya Umma ya Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT) na Askofu Flaviani Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita kwa niaba ya Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Tercius Ngalekumtwa ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa mwishoni mwa wiki Jijini Mwanza.
Dkt. Judith Adongo Aloo akitunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika fani ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT)na Askofu Flaviani Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita kwa niaba ya Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Tercius Ngalekumtwa ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa mwishoni mwa wiki Jijini Mwanza.
Wahitimu wa Shahada ya Uzamivu (PhD) Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT) (mstari wa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa chuo mara baada ya kutunukiwa shahada zao mwishoni mwa wiki Jijini Mwanza. Wa kwanza kulia ni Dkt. Darius Mkiza, wa pili kulia ni Jacob Roman Lubuva, wa kwanza kushoto ni Neema Bhoke Mwita na Judith Adongo Aloo (wa pili kushoto). (Picha na Martin Nyoni, SAUT, Mwanza)
****************************************
Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT) pamoja na Vyuo Vikuu vyake Vishiriki kimetoa jumla ya wahitimu 8,687 kwa mwaka wa masomo 2016/2017 kwa kutekeleza azma ya Serikali ya kuandaa wataalamu mbalimbali nchini. Uongozi wa Chuo hicho umeishukuru Serikali kwa kuishirikisha sekta binafsi katika kutoa mchango wao katika sekta ya elimu na umeihakikishia Serikali kuwa kanisa Katoliki litaendelea kuwa mdau muhimu kwa taifa katika kutoa huduma za jamii nchini.
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Mwanza, ambaye pia alikuwa Mgeni Rasmi katika mahali ya 19 ya chuo hicho ambapo wahitimu hao wametunukiwa Astashahada, Stashahada na Shahada ya kwanza, shahada ya uzamili pamoja shahada ya uzamivu. Askofu Ruwa’ichi amewataka wahitimu hao wawe wabunifu hatua itakayowawezesha kujiajiri na kuwaajiri watu wengine kwa kuitambua na kuitumia vema fursa ya uwepo wa tecknolojia pamoja na fursa nyingine zilizopo katika mazingira na jamii wanapoishi wakizingatia maadili ya taaluma zao pamoja na maadili ya jamii ili waweze kujiletea maendeleo yao wenyewe na taifa kwa ujumla. KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA
“Tambueni na onesheni thamani yenu katika jamii kwa elimu mliyoipata hapa SAUT, jamii inatarajia kutumia ujuzi wenu ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi. Kati ya wahitimu hao, chuo kikuu cha SAUT Mwanza na kituo cha Dar es salaam kimetoa jumla ya wahitimu 2147 ambapo asilimia 55 ni wanaume na asilimia 45 ni wanawake kutoka fani mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo. Fani hizo ni Uandishi wa habari, Mahusiano ya Umma, Mahusiano ya Jamii na Masoko, sosholojia, Falsafa ya Elimu, Uhasibu, Utawala wa Afya, Uchumi, Ugavi, Sheria, Isimu ya Lugha Utawala na Biashara.
Fani nyingine ni, Historia, Utawala wa Elimu na Mipango Usimamaizi wa Maendeleo ya Elimu ya Juu, Uhandisi wa Ujenzi, Sayansi ya Kompyuta, Uhandisi wa umeme, Elimu ya Shule ya Msingi pamoja na Sanaa na Elimu. Miongoni mwa watimu hao wapo wahitimu wane katika ngazi ya shahada ya Uzamivu (PhD) akiwemo Darius D. Mkiza na Jacob Roman Lubuva katika fani ya Mawasiliano ya Umma pamoja na Judith Adongo Aloo na Neema Bhoke Mwita katika fani ya Sheria. Akinukuu maneno ya Rais wa zamani wa Marekani John Kennedy aliyowahi kusema “Usijiulize taifa litakufanyia nini wewe, bali jiulize wewe utalifanyia nini taifa lako”, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwahimiza wahitimu hao wawe wabunifu ili waweze kuonesha tofauti katika jamii kwa kufanya maamuzi sahihi wakati wa kutekeleza majukumu yao na kuwa mabalozi wazuri wa chuo hicho.
Zaidi ya hayo, Askofu Mkuu Ruwa’ichi amewataka wahitimu hao kuwa wakweli daima wakati wa kutekeleza majukumu yao huku akiwahimiza waichukie rushwa, wasitoe wala kupokea rushwa bali wafanye kazi kwa juhudi na maarifa wakimtegemea Mungu daima. Aidha, Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesisitiza kuwa chuo cha SAUT kimekuwa mdau muhimu kwa Serikali ya Tanzania kwa kutoa mchango uliotukuka kwa taifa kwa kuzingatia Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 ambayo ilifanyiwa maboresho ktoka Sera ya Elimu ya mwaka 1995.
Lengo la sera hiyo ni kuiwezesha nchi kupata watanzania walioelimika ili waweze kuingia katika mazingira ya ushindani ili wanaweze kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa viwanda na wa kati ifikapo mwaka 2025 kulingana na Dira ya Maendeleo ya taifa. Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho Padre Dkt. Thadeus Mukama amesema kuwa SAUT imetoa mchango mkubwa taifa katika fani wanazotoa wakiongozwa na fani kongwe ya uandishi wa habari inayotolewa chuoni hapo tangu kuanzishwa kwake.
Dkt. amewataja baadhi ya watumishi mbalimbali waliosoma chuoni hapo na kushika nafasi mbalimbali katika taifa na maeneo mbalimbali duniani wakiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbas, Emmanuel Buhohela, na Jackson Msangulla ambao wanafanyakazi Ofisi ya Rais katika Kurugenzi ya Mawasiliano.
Dkt. Mukama aliendelea kuwataja watumishi wengine waliosoma SAUT kuwa ni pamoja na Deodatus Balile mwandishi wa habari wa gazeti la Jamhuri, Hoyece Temu anayefanyakazi katika Ofisi za Umoja wa Mtaifa, Tanzania, Zawadi Machibya na Sami Awami, Ester Namhisa, Liisy Masinga ambao wanafanyakazi ya uandishi wa habari katika Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC, Raymondi Nyamwihula anafanyakazi Azam Media, Dotto Bulendu anafanyakazi Radio SAUT, Jonas Songora anayefanyakazi radio Japan pamoja na Maafisa Habari na Mahusiano wengi wanaofanyakazi Serikalini katika Wizara, taasisi, mikoa, majiji na halamashauri na mbalimbali zisizo za kiserikali ndani na nje ya nchi.
Aidha, katika mwaka huu wa masomo wa w 2017/2017 Dkt.Mukama amesema kuwa chuo hicho kimedahili wanachuo pamoja na matawi yake kimedahili wanachuo wapatao 20600 ambapo lengo la chuo ni kudahili wanachuo wapatao 30,000 ifikapo mwaka 2020. Kwa upande wao wahitimu wa fani ya Mawasiliano ya Umma Dkt. Darius D. Mkiza na Dkt. Jacob Roman Lubuza ambao pia ni wahadhiri katika Chuo Kikuu cha Tumaini Tawi la Dar es salaam wamesema kuwa watatumia elimu waliyoipaata katika kwa kufundisha vyuo vikuu, kutangaza utalii wa Tanzania, kufanya utafiti, kuandaa mitaala mbalimbali ya elimu na kutoa ushauri wa kitaalam ikiwa ni mchango wao kwa taifa kuelekea kujenga uchumi wa kati.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.