Habari za Punde

LIGI KUU BARA MZUNGUKO WA 12 KUENDELEA KESHO

LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) mzunguko wa 12 katika msimu wa 2017/2018 inaendelea wikiendi hii baada ya kusimama kwa wiki tatu kupisha michuano ya CECAFA iliyofanyika nchini Kenya na mechi za raundi ya pili ya Azam Sports Federation Cup (ASFC).
VPL ambayo wadhamini wenza ni Kituo cha Televisheni cha Azam (Azam Tv) na KCB - Benki inayotoa huduma zake kisasa, itaanza kesho Ijumaa Desemba 29, 2017 kwa mchezo kati ya Azam FC na Stand United kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuanzia Saa 1:00 usiku.
Jumamosi Desemba 30, kutakuwa na michezo mitatu - Lipuli na Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Samora mkoani Iringa kuanzia saa 8:00 mchana; Mtibwa Sugar na Majimaji ya Songea katika dimba la Manungu, Turiani mkoani Morogoro ilihali Ndanda itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona - Mtwara. Mechi hizo mbili zitachezwa kuanzia saa 10:00 jioni.
Jumapili, mabingwa watetezi wa VPL, Young Africans watakuwa wageni wa Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni huku Njombe Mji FC na Singida United wakitangulia kwa mchezo utakaoanza 8:00 mchana Uwanja wa Saba Saba, Njombe.
VPL itakamilisha mechi za mzunguko wa 12 katika mechi zitakazopigwa mwakani, Januari mosi ambako Mbeya City wakiikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Mwadui wakiikaribisha Ruvu Shooting zote kuanzia saa 10:00 jioni.
Baada ya mechi hizo, Ligi Kuu itasimama tena kupisha mechi za Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar na raundi ya tatu ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani kabla ya kuingia kwenye mzunguko wa 13 wa ligi kuanzia Januari 13 na 17, 2018.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.