Habari za Punde

RAIS MAGUFULI ATOA MSAMAHA KWA WAFUNGWA 61 WA ADHABU YA KIFO, BABU SEYA NA PAPII KOCHA

 Makomandoo wakionyesha umahiri wao wa kushuka kwa kamba kutoka katika Helkopta baada ya kumuokoa kiongozi aliyetekwa.
 Askari wa JWTZ Makomando wakipita mbele ya jukwaa kuu na kutoa heshima.  
*********************************************
Na Ripota wa Mafoto Blog, Dodoma
RAIS Dk. John Magufuli, ametoa msamaa kwa wafungwa 61 waliohukumiwa adhabu ya kifo pamoja na kuwaachilia huru wanamuziki maarufu Nguza Viking (Babu Seya) na mwanae Johnson Nguza (Papii Kocha).
Wanamuziki hao walihukumu kifungo cha maisha gerezani na Mahakama Kuu, mwaka 2004 baada ya kupatikana na hatia ya kubaka na kulawiti wasichana 10 wa shule ya Msingi Mashujaa wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.
Hukumu hiyo ilizua hisia tofauti nchini huku idadi kubwa ya wananchi wakiamini kuwa, wanamuziki hao wakuhusika na tukio hilo.
Hata hivyo Novemba 21 mwaka 2013, Mahakama ya Rufaa ilitupilia mbali ombi la Babu Seya na Papii Kocha ambao waliomba mahakama hiyo kufanya marejeo ya uamuzi wake wa awali wa kuwapata na hatia kama ambavyo hukumu dhidi yao ilivyotolewa. KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA

Mahakama hiyo baada ya kufanya mapitio ikiwa imeketi chini ya majaji watatu, iliamua warufani hao wawili wanahatia hivyo waeendelee kutumikia adhabu yao.
Akitumia Ibara ya 45 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotoa mamlaka kwa rais kutoa msamaa kwa wafungwa, Rais Dk. Magufuli alitangaza kutoa msamaa kwa Babu Seya na mwanaye kwenye sherehe za miaka 56 ya uhuru wa Tanzania Bara, iliyofanyika jana, katika uwanja wa Jamhuri mjini hapa.
“Sisi sote ni binaadamu na hata mimi huwa namuomba Mungu anisamehe, ingawa sisi wanadamu ni wagumu kusamehe. Hivyo natangaza msamaha kwa familia ya Nguza Viking maarufu kama Babu Seya na watoke leo,” alisisitiza, Rais huku akishangiliwa na umati wa watu waliohudhuria sherehe hizo.
Kuhusu wafungwa 61 waliohukumiwa adhabu ya kifo, Rais alitangaza kuwasamehe kutokana na kukaa gerezani kwa miaka mingi.
Alisema baada ya kufanyika uchunguzi imegundulika wafungwa hao wamejutia makosa yao kwa kiasi kikubwa na wamejirekebisha.
“Yupo mtu alifungwa akiwa na miaka 18. Sasa ana umri wa miaka 60 akiwa gerezani. Mwingine Mganga Matonya mwenye umri wa miaka 87 ambaye amekaa gerezani kwa miaka 44.
“Nitamkabidhi Waziri Mkuu orodha ya wafungwa wote ili ahakikishe utaratibu unafanyika wakuachiwa huru leo au kesho. Nahii document (nyaraka) naisaini hapa hapa. Lisiongezwe jina lingine au kupunguzwa,” alibainisha.
Alisema wafungwa hao 61 hawakuua watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) wala kuhusika na vitendo vya ujambazi, lakini alisisitiza serikali kuendelea kusimamia sheria kwani uwepo wa ibara hiyo ya kikatiba aina maana sheria haitofuata mkondo.
Rais alitaja idadi ya wafungwa waliosamehewa ambapo kwenye gereza la Uyui (2), Butimba (5), Ukonga (19), Isanga (15), Maweni (11) Kinguwila (5) na gereza la Ruanda wapo wafungwa wanne.
Pia rais alitoa msamaha kwa wafungwa 8,157 ambao kati yao 1,828 walitakiwa kutoka tangu jana na wengine 6,329 walipunguziwa muda wa kukaa gerezani.
Akitoa takwimu ya idadi ya wafungwa waliopo magerezani, rais alisema hadi juzi kulikuwa na wafungwa 39,000 kati yao wafungwa 37,000 ni wanaume na wanawake ni wafungwa 2,000.
Dk. Magufuli alieleza wafungwa waliohukumiwa kunyongwa ni 522 kati yao wanaume 503 na wanawake 19.
Alisema wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha ni 666 kati yao wanaume 655 na wanawake 11.
“Kwa maana hiyo wafungwa wengi waliopo magerezani ni wanaume, hivyo tuanze kujitambua ni kwanini wanaume wanaongoza kwenye vitendo vya uhalifu.
MAFANIKO BAADA YA UHURU
Rais alisema mara baada ya uhuru nchi imepiga hatua kubwa za maendeleo licha ya baadhi ya watu kutokubaliana na ukweli huo.
Alisema kabla ya uhuru kulikuwa na kilomita 33,600 za barabara ambapo kati ya hizo kilomita 1,360 ndizo zilikuwa za lami, lakini baada ya miaka 56 ya uhuru nchi ina kilomita za barabara 122,500.
“Kati ya hizo kilomita 80,000 zipo chini ya Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA), 36,000 zipo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na barabara 6,500 zipo chini ya mamlaka za wanyamapori.
Dk. Magufuli alisema kilomita 12, 676 zimekwisha wekewa lami na zingine 2,480 zipo kwenye hatua mbalimbali ya kuwekewa lami.
Rais alieleza hadi sasa madaraja makubwa 17 yameshajengwa huku vituo vya afya 7,293 vinatoa huduma kwa wananchi ikilinganishwa na vituo 1,095 vilivyokuwepo kabla ya uhuru.
Kwa upande wa shule za msingi, alisema kabla ya uhuru zilikuwepo 3,100 ambapo sasa shule za msingi zilizopo ni 17,375, sekondari zilikuwa 41 na sasa zipo 4,817 na vyuo vikuu vimefikia 48 kutoka kimoja.
Alisema waandisi wa Kiafrika walikuwa wawili kabla ya uhuru na sasa wamefiki 19,164 huku wakandarasi wamefikia 9,350 kutoka wawili.
Pia alibainisha wastani wa kuishi kabla ya uhuru ulikuwa miaka 37 na sasa umefikia miaka 61 huku idadi ya watu ikiongezeka kutoka milioni tisa hadi milioni 52.
Rais alitoa misisitizo wa azma ya serikali kuhamia Dodoma akieleza kuwa mwakani atahamia rasmi na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, yupo kwenye hatua za mwisho kuhamia kwenye makao makuu ya nchi.
“Hata sherehe hizi za uhuru zitaendelea kufanyika Dodoma kwakuwa ndipo makao makuu ya nchi. Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya mji wa Dodoma,” alisema.
Aliwataka wananchi kuendelea kuulinda uhuru, umoja, amani na muungano huku akionyesha kutamani kushuhudia sherehe kama hizo akiwa rais mstaafu kama ambavyo marais wengine wa awamu zilizopita wanavyofanya.
“Hili linawezekana kwa Tanzania tuu..!! Sehemu nyingine ni jambo gumu na haliwezekani kabisa,” alisisitiza.
HALI ILIVYOKUWA
Sherehe hizo ziliwavutia idadi kubwa ya wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani ambao walijitokeza kwenye uwanja wa Jamhuri kuanzia saa 12 asubuhi.
Hadi saa 1: 49 asubuhi, uwanja huo ulikuwa umejaa na kuwalazimu baadhi ya watu kuketi nje ya uwanja huo mahali palipofungwa runinga ilioonyesha kile kinachoendelea ndani ya uwanja.
Mara baada ya gwaride kuingia uwanjani saa 1:48 asubuhi, viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa walianza kuwasili akiwemo Makamu wa rais, Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Spika wa Bunge Job Ndugai.
Wengine ni rais mstaafu Jakaya Kikwete, Benjamin Mkapa, Ali Hassan Mwinyi, mawaziri, mabalozi, wabunge na wawakilishi wa vyama vya siasa.
Sherehe hizo zilipambwa na gwaride kutoka vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama, kikosi maalum cha komando kilichoonyesha umahiri wa kuokoa watu kwa kutumia helkopta, onyesho la askari wa pikipiki, gwaride la uzalendo na vikundi vya sanaa na burudani.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli, akipunga mkono kuwasalimia wananchi wakati akiwasili kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma jana kuongoza sherehe za kuadhimisha miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara. 
 Sehemu ya viongozi na wageni waalikwa wakishuhudia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza  sherehe za kuadhimisha miaka 56 ya Uhuru katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma leo.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa, Mama Janeth Magufuli na Mama Mwanamema Shein kwenye sherehe hizo
Marais wastaafu, aLI Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, wakiteta jambo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa sherehe za kuadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

 Sehemu ya viongozi na wageni waalikwa wakishuhudia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza  sherehe za kuadhimisha miaka 56 ya Uhuru katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma leo
  Sehemu ya viongozi na wageni waalikwa wakishuhudia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza  sherehe za kuadhimisha miaka 56 ya Uhuru katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma leo 
 Sehemu ya viongozi na wageni waalikwa wakishuhudia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza  sherehe za kuadhimisha miaka 56 ya Uhuru katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma leo 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.