Habari za Punde

VIONGOZI WAKUU TFF KUMZIKA BENDERA

Viongozi wakuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Rais Wallace Karia na Makamu Rais Michael Wambura wataongoza ujumbe wa shirikisho katika mazishi Kocha wa zamani wa Taifa Stars, marehemu Joel Nkaya Bendera.
Bendera aliyefariki dunia Desemba 6, mwaka huu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, atazikwa leo Jumapili Desemba 10, 2017 makaburi ya Kijiji cha Manundu, Korogwe mkoani Tanga.
Ujumbe huo pia utamjumuisha Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la TFF, Mhe. Mohammed Abdulaziz; Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi; Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Vedastus Lufano pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Kanda ya 12 (Mikoa ya Tanga na Kilimanjaro), Khalid Mohammed.
Khalid Mohammed atakuwa na wenyeji wengine ambao ni viongozi wa mpira wa miguu mkoa na wilaya za Tanga ambao wataungana familia pamoja na waombolezaji wengine kumpumzisha Mbunge huyo wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1995 hadi 2005) katika Jimbo la Korogwe Mjini.
Mwili wa marehemu Bendera umeagwa Jumamosi Desemba 9, mwaka huu asubuhi kwenye Viwanja vya Hospitali ya Jeshi la Lugalo, Dar es Salaam.
Enzi zake Joel Nkaya Bendera alifikia cheo cha Naibu Waziri Michezo mbali ya kuongoza mikoa ya Morogoro na Manyara kwa cheo cha Mkuu wa mkoa.
Anakumbukwa zaidi kuwa sehemu ya benchi la ufundi lenye mafanikio kuingoza timu ya soka ya Tanzania kuiondoa Zambia na Tanzania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa Huru ya Tanzania mwaka 1979.
Taifa Stars ilishinda bao 1-0 dhidi ya KK Eleven ya Zambia (sasa Chipolopolo) na kuifanya Tanzania kushiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo mikubwa Afrika kwa upande wa timu za taifa iliyofanyika Nigeria. Taifa Stars haijafuzu tena katika michuano hiyo.
Joel Bendera – ndiye aliyeiongoza Simba kushinda mabao 5-0 dhidi ya Mufulira Wondereres huko Zambia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1979.
Ikumbukwe kwamba Simba ilifungwa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza ulifanyika Dar es Salaam.
Joel Bendera – ndiye aliyeiongoza Coastal Union ya Tanga kutwaa ubingwa wa Bara na kucheza michuano ya Afrika Mashariki na Kati na kuifikisha timu hiyo fainali. Wakati akifanya kazi na hayati Zacharia Kinanda.
Joel Bendera – akiwa Naibu Waziri Michezo, chini Waziri George Huruma Mkuchika ndiye aliyeihamaisha Taifa Stars kucheza vema hadi kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), mwaka 2009.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.