Habari za Punde

WATOTO 130 WENYE MATATIZO YA MOYO WAFANYIWA UCHUNGUZI KATIKA KAMBI YA MATIBABU TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE (JKCI)

Na Mwandishi wetu
Jumla ya watoto 130 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa uchunguzi katika kambi maalum ya matibabu inayoendelea katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Matibabu hayo yanafanywa na Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa watoto wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa mradi wa Little Hearts wa nchini Saudi Arabia ambao ni moja ya mradi wa Afya ulioko ndani ya Taasisi ya Msaada ya Muntada yenye makao Makuu yake mjini London nchini Uingereza.
Akiongea na waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa watoto Naiz Majani alisema kati ya watoto waliofanyiwa uchunguzi watoto 36 wamefanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua na 18 wamefanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na hali zao zinaendelea vizuri.
Dkt. Naiz alisema watoto waliofanyiwa uchunguzi na kufanyiwa upasuaji ni wale ambao mioyo yao ina matundu na mishipa ya damu ya moyo haipitishi damu vizuri.
“Katika kambi hii tunatarajia kufanya upasuaji kwa watoto 80 kati ya hao watakaofanyiwa upasuaji wa kufungua kifua ni 30 na bila kufungua kifua ni 50 na watoto watakaobaki watafanyiwa upasuaji na Madaktari wetu”, alisema.
Aliitaja changamoto kubwa wanayokabiliana nayo katika kambi hiyo ni upatikanaji wa damu na kuwaomba wananchi wazidi kujitokeza kwa wingi kuchangia damu kwani mgonjwa anayefanyiwa upasuaji wa moyo anatumia kati ya chupa sita hadi saba za damu.
Kwa upande wake Paulina Egbert ambaye mtoto wake amefanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua alisema mtoto alikuwa na tatizo la kukohoa baada ya kumfanyiwa kipimo mwezi wa tatu mwaka huu Madaktari wakagundua moyo wake una tundu.
Paulina aliishukuru Serikali kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kutoa huduma ya matibabu ya Moyo hapa nchini na kuongeza kuwa ingekuwa miaka ya nyuma kupata huduma ya matibabu ingechukuwa muda mrefu lakini kwa sasa mgonjwa akigundulika na matatizo anatibiwa kwa wakati.
Watoto waliofanyiwa uchunguzi na kupata matibabu ya upasuaji katika kambi hiyo ya siku sita ni wale wenye umri wa mwaka mmoja hadi miaka kumi na nne.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.