Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (wa tatu kulia), akiwa katika
picha ya pamoja na Uongozi wa Shirika la Ndege la FlyDubai, mara baada Waziri
huyo kuzindua safari za shirika hilo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro (KIA), Mkoani Kilimanjaro leo. Katikati ni Makamu wa Rais
Uendeshaji Biashara wa Shirika hilo, Sudhir Sreedharan.
Ndege ya Shirika la Ndege la FlyDubai, ikiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), na kupewa heshima ya kumwagiwa maji ikiwa ni safari yake ya kwanza katika uwanja huo.
Wageni waalikwa
wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa
(hayupo pichani), wakati akitoa hotuba yake wakati wa uzinduzi wa safari za Shirika
la Ndege la FlyDubai katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA),
Mkoani Kilimanjaro leo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (wa pili kulia), Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mgwira (kulia), Makamu wa Rais Uendeshaji Biashara wa Shirika la Ndege la FlyDubai, Sudhir Sreedharan (wa pili kushoto), wakikata keki kuashiria uzinduzi rasmi wa safari za Ndege za Shirika hilo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Mkoani Kilimanjaro leo.
Makamu wa Rais Uendeshaji Biashara wa Shirika la Ndege la FlyDubai, Sudhir Sreedharan, akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, madaraja mbali mbali yaliyoko kwenye ndege ya Shirika hilo, wakati wa uzinduzi rasmi wa safari zake katika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Mkoani Kilimanjaro leo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Eng, Christopher Mukoma, akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika jengo la abiria katika uwanja huo, Mkoani Kilimanjaro leo.
************************************
SERIKALI imesema
itahakikisha inatoa ushirikiano kwa Shirika la Ndege la Dubai(Fly Dubai),
kuhakikisha kwamba inafanya kazi zake vizuri za utoaji wa huduma za usafiri wa
anga hapa nchini.
Akizungumza leo mkoani
Kilimanjaro katika uzinduzi wa safari za ndege kutoka Uwanja wa ndege wa
Kilimanjaro (KIA) kuelekea nchini Dubai, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amesema kuwa uzinduzi wa safari hizo
utakuza sekta ya utalii na biashara mkoani humo na nchi kwa ujumla.
"Naamini kupitia
uzinduzi huu uchumi wetu utakua kwani wafanyabiashara na watalii kutoka nchi
mbalimbali wataweza kuongezeka zaidi sababu wamesogezewa huduma za usafiri wa
ndege za kimataifa katika viwanja vya ndege vikubwa nchini", amesema
Waziri Prof. Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa
ameuhakikishia uongozi wa shirika hilo la ndege kuwa hawatojutia uamuzi wao wa
kuamua kusogeza huduma zao za usafiri katika uwanja huo kwani wafanyabiashara
wengi na wananchi kutoka sehemu mbalimbali wamekuwa wakitumia uwanja huo.
Kwa upande wake Makamu
wa Rais wa Shirika la ndege la Dubai, Sudhir Sreedharan, amesema kuwa kutokana
na umuhimu na ubora wa uwanja huo wameamua kusogeza huduma zao kutokana na
kuamini kuwa wageni wengi wa kimataifa wamekuwa wakitumia uwanja huo kwenda
sehemu mbalimbali za vivutio vya utalii mkoani humo na mikoa ya jirani ya
Arusha na Manyara.
"Kuna mambo mengi yametuvutia kuanzisha safari zetu katika uwanja huu,
tunaamini hata soko letu la biashara litafanikiwa kwa kuongeza huduma
hapa", amefafanua Makamu wa Rais.
Shirika la ndege la
Dubai, sasa litatoa huduma za usafiri wa anga katika viwanja vya ndege vitatu
kikiwemo kilichozinduliwa leo cha KIA na vile viwanja viwili vya ndege vya
Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) na Uwanja wa ndege wa Zanzibar vilivyokuwa awali.
No comments:
Post a Comment