Habari za Punde

RAIS WA FIFA AITUNUKU TANZANIA, KUTUA DAR FEBRUARI

UNAWEZA kusema ni neema kubwa kwa Tanzania. Sekta ya michezo nchini inakaribia kupata neema kubwa ambayo kila nchi ya Afrika inaihitaji. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limepata uenyeji wa mkutano mkuu wa mwaka wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), unaotarajiwa kufanyika Februari 22 mwaka huu.
Mkutano huo unaotambulika kwa jina la FIFA Summit utakuwa na kauli mbiu inayotajwa 'FIFA Foward' ambapo utafanyika katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC).
Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Wallace Karia, alisema mkutano huo utahudhuriwa na Rais wa FIFA, Gianni Infantino ambaye ataufungua na kuufunga kwa ajili ya kujadili maendeleo ya soka.
Alisema marais na makatibu wakuu wa mashirikisho ya soka katika nchi 19 barani Afrika na rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad Ahmad watahudhuria katika mkutano huo mkuu.
Alisema mkutano huo utakuwa na ajenda kuu nne ambazo zitasaidia kuendeleza soka Afrika ikiwemo kutolewa kwa dola milioni 2 kwa kila mwaka katika nchi wanachama wa FIFA.
Karia alisema mkutani huo utakuwa na faida kwa Tanzania katika michuano ya vijana na wanawake ambapo mbali na hilo FIFA itajidili uboreshwaji wa viwanja katika soka la Tanzania na nchi zitakazoshiriki.
Alisema mkutano huo utajadili kalenda ya michuano ya FIFA na CAF katika kuweka kwenye ratiba za Ligi na mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao (TMS).
Karia alisema ni faraja kubwa kwa Tanzania na Shirikisho lake kupata uenyeji huo ambao ni ugeni mkubwa.
Aidha Karia alisemA mbali na TFF kufurahia nafasi hiyo, pia ni fursa ya kipekee kwa Wizara ya Maliasili na utalii katika kuhakikisha Tanzania inafaidika na ujio huo.
"Tunatarajia kuwa na ugeni kutoka FIFA ukiongozwa na rais Infantoni, hii ni fursa kubwa kwa Tanzania kwa kuwa nchi nyingi zimehitaji nafasi hii lakini imeshindwa kuipata," alisema Karia.
Nchi zitakazoshiriki Mkutano huo ni Tanzania ambayo ndio wenyeji, Algeria, Mali, Morocco, Burkina Faso, Angola, Niger, Bahrain, Palestina, Saudi Arabia (UAE), Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ivory Coast, Tunisia, Bermuda, Monserrat, St. Lucia, Visiwa vya US Virgin, Maldives na DR Congo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.