Habari za Punde

YANGA YAIBUKIA KWA MASAO BWIRE WA RUVU SHOOTING

Wachezaji wa Yanga wakimpongeza Pius Buswita baada ya kuifungia timu hiyo bao pekee katika mchezo wa leo. 
*************************************
LILIKUWA ni bao pekee la dakika ya 45 ndani ya dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza la Kiungo wa Yanga, Pius Buswita katika mchezo wa leo dhidi ya Ruu Shooting, limeiwezesha Yanga kufikisha jumla ya Pointi 25 na kurudisha morali kwa timu hiyo ambayo ilipoteza mchezo na Mbao fc na kutoka sare na Mwadui.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika huku Yanga wakiwa mbele kwa bao hilo la Buswita lililodumu hadi kumalizika dakika 90 za mchezo huo uliokuwa umetawaliwa zaidi na ubabe na rafu za mara kwa mara.
Dakika moja kabla ya Buswita kufunga, Ayoub Kitala aliikosesha Ruvu bao la wazi baada ya kupiga mpira juu ya lango akiwa amebaki yeye na nyavu baada ya kipa wa Yanga kupotea maboya akijaribu kumalizia krosi ya Abdulrahman Mussa aliyewachambua mabeki wa Yanga.
Mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajib (kulia) akimpita beki wa Ruvu Shooting.
Kiungo wa Yanga, Pius Buswita (katikati) akipasua katikati ya wachezaji wa Ruvu Shooting
Beki wa Yanga, Hassan Kessy akimtoka beki wa Ruvu Shooting, Mau Bofu na kupiga krosi
******************************
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Florentina Zabron kutoka Dodoma aliyesaidiwa na Rashid Zongo wa Iringa na Michael Mkongwa kutoka Njombe, Yanga walikianza vizuri kipindi cha pili na kiungo aliyechezeshwa kama sentahafu leo, Said Juma ‘Makapu’ aliunganishia kwenye nyavu za nje kwa kichwa kona ya Ajib.
 Yohana Nkomola (kulia) akichezewa rafu........
 Raphael Daud akijaribu kukatiza katikati ya mabeki wa Ruvu Shooting
 KIUNGO wa Yanga Raphael Daud (katikati) akiwatoka wachezaji wa Ruvu Shooting, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
 Bekiwa Yanga Haji Mwinyi (kulia) akijaribu kumtoka beki wa Ruvu Shooting, Jabdulrhman Mussa, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 
 Kiungo wa Yanga, Papy Tshishimbi, akipiga pasi, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 
Ajib akimchekecha beki Ruvu Shooting
*****************************
Buswita akapiga shuti la umbali wa mita 20 dakika ya 62 baada ya kupokea pasi ya kiungo Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi, lakini likaenda nje. 
Almanusra Issa Kanduru aisawazishie Ruvu dakika ya 64 baada ya kuwachambua vyema mabeki wa Yanga na kumpiga chenga kipa Mcameroon, Youthe Rostand lakini akachelewa kufunga hadi beki Hassan Kessy akatokea na kuokoa bao la wazi.
Jamal Soud aliyeingia kuchukua nafasi ya Adam Ibrahim naye alikaribia kuipatia bao Ruvu bao la kusawazisha kwa shuti la mbali dakika ya 79, lakini mpira ukatoka nje.
Juma Mahadhi naye aliyeingia kuchukua nafasi ya Amissi Tambwe kipindi cha pili, akapoteza nafasi nzuri ya kjfunga baada ya kuingiziwa krosi safi na Emmanuel Martin, lakini akapiga nje.
Yanga inafikisha pointi 25, baada ya kucheza mechi 14 na kupanda hadi nafasi ya tatu, nyuma ya Simba SC yenye pointi 29 na Azam FC pointi 30. 
Mzunguko wa 14 wa Ligi Kuu utakamilishwa kesho kwa mechi mbili, Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera Sugar wataikaribisha Simba SC na Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, Maji Maji watakuwa wenyeji wa Singida United. 
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Azam FC imeshinda 2-0 dhidi ya wenyeji, Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya mabao yake yakifungwa na Yahya Zayed dakika ya 24 na Paul Peter dakika ya 82, wakati Mwadui FC imelazimishwa sare ya 1-1 na Ndanda FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga wageni wakitangulia kwa bao la John George dakika ya 43 kabla ya Awadh Juma kuwasawazishia wenyeji dakika ya 48.
Kikosi kamili cha Yanga leo kilikuwa; Youthe Rostand, Hassan Kessy Mwinyi Hajji Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’, Said Juma ‘Makapu’, Papy Kabamba Tshishimbi, Pius Buswita, Raphael Daudi/Pato Ngonyani dk86, Amissi Tambwe/Juma Mahadhi dk69, Yohanna Nkomola/Emmanuel Martin dk28 na Ibrahim Ajib.

Ruvu Shooting; Abdallah Rashid, George Amani, Mau Bofu, Damas Makwaya, Rajab Zahir, Baraka Mtui, Abdulrhaman Mussa, Adam Ibrahim/Jamal Soud dk46, Issa Kanduru, Shaaban Msala, Ayoub Kitala/Fully Zully Maganga dk49.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.