Habari za Punde

YANGA YAMWAGA WINO NA KAMPUNI YA MARCON MIAKA MITATU


Na Tima Sikilo, Dar
KLABU ya Yanga leo  imesaini mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya sh. Bilioni 2 na Kampuni ya Marcon kutoka Italia kwa ajili ya utengenezaji na uuzaji wa jezi za klabu hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini mkataba huo leo makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Jangwani, Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Yanga, Charse Boniphace Mkwasa amesema, mkataba utakuwa na ongezeko kutokana na makubaliano waliyofikia. 
Aidha alisema kuwa dau litakuwa likiongezeka kulingana na idadi ya mauzo ya jezi za mashabiki.
Kampuni hiyo mwezi Desemba mwaka jana, walisaini mkataba wa miaka miwili na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa udhamini wa jezi za timu zote za taifa zikiwemo za vijana na wakubwa kwa wanawake na wanaume wenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 800.
Baada ya hafla hiyo Mkwasa aliwaasa wale wanaouza jezi mitaani kwa manufaa yao binafsi ambayo hayainufaishi klabu yao waache mara moja.
"Kwa wataoendelea na biashara hiyo watachukuliwa hatua,"amesema Mkwasa.
Kwa upande wa Mkurugenzi kampuni ya Marcon Tanzania, Suleiman Karimu ameishukuru klabu ya Yanga kwani makubaliano hayo yataleta mapinduzi ya mpira wa miguu hapa nchini.
Katibu Mkuu wa Yanga Boniface Charles Mkwasa (kushoto) akisainiana  mkataba na Mkurugenzi wa Kampuni ya Macron Tanzania, Suleiman Karim 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.