Habari za Punde

HAFLA YA MAHAFALI YA 16 YA CHUO CHA BANDARI LEO

  Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, akimkabidhi cheti mmoja kati ya wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao, Mercy Masawe, wakati wa hafla ya Mahafali ya 16 ya Chuo cha Bandari yaliyofanyika chuoni hapo jijini Dar es Salaam, leo.
 Mgeni rasmi akikabidhia zawadi...
 Mgeni rasmi  Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, akihutubia katika hafla hiyo, ambapo ametoa muda waa mwezi mmoja kwa waliohusika kuchukua sehemu ya maeneo ya Chuo hicho na kuwakabidhi Chuo cha Utalii.
*************************************************
*NDITIYE: BANDARI ITOE NAFASI YA MAFUNZO KWA VITENDO KWA WANACHUO
NAIBU Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye ameilekeza Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) pamoja na uongozi wa Menejimenti wa Mamlaka hiyo kutoa nafasi kwa wanachuo wa Chuo cha Bandari Dar es Salaam kufanya mafunzo kwa vitendo wakati wa masomo yao kwenye bandari zote nchini.
Mhandisi Nditiye ameyasema hayo akiwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 16 ya Chuo cha Bandari Bar es Salaam ambapo jumla ya wahitimu 521 wametunikiwa cheti cha kuhitimu mafunzo yao katika ngazi ya elimu ya astashahada na stashahada ya mafunzo ya aina mbalimbali ikiwemo mafunzo ya usimamizi wa shughuli za meli na bandari; uhandisi na usimamizi wa matengenezo; zimamoto na usalama; masoko na mawasiliano ya umma; usimamizi wa wakala wa forodha na usafirishaji wa mizigo; usimamizi wa mipango ya uchukuzi na usafirishaji; na utawala na biashara.
Ameongeza kuwa nia ya Serikali ni kufikia malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya kuboresha bandari zetu, kuongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi wa sekta ya usafirishaji majini ili kukuza uchumi na kuongeza mapato la taifa letu.
Pia, wakati akisoma hotuba yake kwa wahitimu hao, Mhandisi Nditiye amewataka wahitimu hao kutumia vyeti vyao na taaluma waliyoipata vizuri kwa kukitangaza vema Chuo cha Bandari Dar es Salaam aidha kwa kujiajiri au kuajiriwa ndani na nje ya nchi. Aidha, amesisitiza kuwa wanaoajiriwa kuwa wafanyakazi wa bandari mbalimbali wawe wamehitimu chuo na kuwa na elimu inayotakiwa. Vile vile amemuagiza Mkuu wa Chuo cha Bandari Dkt. Joseph R. Kakeneno kujenga zahanati kwa ajili ya kutoa huduma za tiba kwa wanachuo na jamii ya Chuo hicho.
Naye mjumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamzi wa Bandari Tanzania mzee Renatus Mkinga ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa bodi wa Mamlaka hiyo Prof. Ignas Rubalatuka, katika mahafali hayo amewataka wanachuo kusoma kwa bidii ili waweze kuajiriwa na kufanya kazi mahali popote iwe ndani au nje ya nchi.
Aidha, wahitimu wa chuo hicho wamemshukuru Dkt. Kakeneno kwa kufanikisha upatikanaji wa ithibati sita za kozi mbalimbali kati ya ithibati nane zinazohitajika. Hivyo, wamemuomba mgeni rasmi Mhandisi Nditiye kumsaidia Dkt. Kakeneno kupata ithibati nyingine mbili zilizosalia.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Nditiye ametoa mwezi mmoja kwa Chuo cha Bandari Dar es Salaam kwa kushirikiana na wataalamu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kurudisha majengo ya Chuo hicho, uwanja wa michezo na mali zote zilizokuwa zinatumiwa na Chuo cha Hoteli na Utalii ambazo ziko ndani  ya eneo la Chuo cha Bandari ya Dar es Salaam yarudishwe kwenye Chuo cha Bandari.
 Baadhi ya wahitimu wakimsikiliza mgeni rasmi
 Baadhi ya wahitimu waliosimama (nyuma) wakitunukiwa astashahada zao 
 Vyeti kwa wanafunzi waliofanya vizuri kimasomo
Picha ya pamoja na mgeni rasmi baada ya kuwatunuku wahitimu

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.