Habari za Punde

WILAYA TANO ZITAKAZOFANYA VIZURI UJENZI WA VITUO VYA AFYA KUPATA TUZO

Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amesema wilaya tano zitakazofanya vizuri katika ujenzi wa vituo vya afya unaoendelea hapa nchini zitapewa vyeti na kutangazwa.
Jafo aliyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya uongozi kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa wilaya yaliyofanyika Mkoani Dodoma mwanzoni mwa mwezi huu.
“Nendeni mkashindane mpate matokeo makubwa, kufikia Aprili 30 mwaka huu tuone vituo vya afya vimekamilika. Wilaya Tano zitakazo fanya vizuri zaidi katika ujenzi wa vituo vya afya zitapewa zawadi na kutangazwa,” alisema Jafo.
Aliendelea kusema kuwa Wilaya 10 zitakakofanya vibaya zitatangazwa pia, aidha amesema ni imani yake kuwa wilaya zote zitafanya vizuri katika ujenzi huo.
“Lakini hata kama wilaya zote zitafanya vizuri basi zitatangazwa kuwa zimefanya vizuri,” alifafanua Jafo.
Jafo ameuelezea ujenzi huo kuwa ni ujenzi mkubwa kufanyika nchini tangu nchi ipate uhuru ambapo zaidi ya vituo vya afya 200 vinajengwa nchi nzima. Vituo hivyo vinatarajiwa kukamilika ifikapo Aprili 30 mwaka huu vikiwa na lengo la kupunguza vifo vya kina mama na watoto hasa maeneo ya vijijini.
Hivyo basi Jafo amewataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi hao kupitia mafunzo ya uongozi waliyoyapa wakatekeleza kwa vitendo usimamizi wa ujenzi wa vitu hivyo ili viweze kukamilika kwa wakati na wananchi waweze kupata huduma za matibabu haraka iwezekanavyo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.