Habari za Punde

YANGA INAVYOZIDI KUFUKUZA MWIZI KIBISHOO ‘KAMATA MWIZI BAAB’

Na Ripota wa Mafoto Blog, Dar 
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga leo tena wameonyesha kuwa bado wanazidi kuinadi staili yao ya kufukuza mwizi kimyakimya baada ya kuendeleza ushindi kwa kuichapa Stand United kwa mabao 3-1 na kufikisha pointi 46 sawa na Watabi zao Simba wanaoongoza ligi hiyo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. 
Katika mchezo wa leo Yanga ilishuka dimbani, ikiwa na pointi 43, baada ya mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar, leo ilionekana kuwadhibiti wapiga debe wa Stand United kwa kuduwaza kwa mabao ya mapema. 
 Hata hivyo mabao mengi ya Simba yenye mechi moja mkononi ya Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kucheza michezo 20 na Yanga 21, yamezuia mabingwa hao watetezi wa ligi kuu kukaa kileleni, huku Simba wakiwa na mabao 49 na Yanga 38. 
Mchezo ulianza kwa kasi ambapo dakika ya sita Yanga walipata bao la kuongoza baada ya mchezaji wa Stand United, Ally Ally kujifunga wakati akiokosa shuti la Yusuph Mhilu.
  Wakitandaza kandanda safi Yanga walipata bao la pili dakika ya 12 likiwekwa kimiani na Ibrahim Ajib baada ya kupokea pasi murua ya Maka Edward 
Mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa nusura aipatie timu yake bao jingine dakika ya 35 baada ya kuingia na mpira kwenye eneo la hatari, lakini shuti lake lilitoka nje. 
 Dakika ya 44, Stand walifanya shambulizi la kushtukiza ambapo Bigiramana Blaise alipiga shuti nje ya eneo la hatari mpira ukatoka nje kidogo ya lango, ambapo Yanga walienda mapumziko wakiwa mbele mabao 2-0 dhidi ya Stand. 
Yanga walifanya shambulizi jingine dakika ya 48, Ajib alipata nafasi nzuri na kushindwa kuitumia baada ya kupiga kombora ambalo lilipaa juu. 
 Dakika ya 65 Stand United walijibu shambulizi, ambapo Aron Lulambo alipiga shuti lililogonga mwamba na kurudi mabeki wakaokoa hatari hiyo. 
Stand United walionekana kulisakama lango la Yanga mara kwa mara ambapo dakika ya 70, Bigiramana alipiga shuti lililoishia kwenye mikono ya kipa Youthe Rostand. 
 Mwamuzi Clemence Manga wa Njombe, alimpa kadi ya njano Pius Buswita dakika ya 71 baada ya kupinga uamuzi wake. 
Stand United walipata bao la kufutia machozi dakika ya 84 kupitia kwa Vitalis Mayanga baada ya kumalizia pasi ya Aron Lulambo. 
 Bao hilo halikudumu kwani dakika moja tu baadaye Yanga waliongeza la tatu lililofungwa dakika ya 85 na Chirwa ambaye alimtoka beki wa Stand United na kuachia fataki kali lililomshinda kipa Mohamed Makaka wa Stand na kutinga wavuni.
  Chirwa sasa amefikisha mabao 12 katika vita ya kuwania kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu Tanzania Bara akimfuatia kinara Emmanuel Okwi mwenye mabao 16.
Yanga: Youthe Rostand, Juma Abdul, Gadiel Michael, Said Juma, Kelvin Yondani, Maka Edward, Yusuph Mhilu, Pius Buswita, Obrey Chirwa, Raphael Daud/Juma Mahadhi na Ibrahim Ajib/Emmanuel Martin. 


Stand United: Mohamed Makaka, Aron Lulambo, Miraji Maka/Makenzi Kapinga, Ally Ally, Erick Mulilo, Jisend Mathias/Ismail Gambo, Bigiramana Blaise, Abdul Swamad, Tariq Seif, Ndikumana Seleman na Vitalis Mayanga.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.