Habari za Punde

YANGA NI MWENDO WA KIMYA KIMYA, YAIPA KAGERA SUGAR 3-0


MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wameendelea kukufua matumaini ya kutetea ubingwa wao na kuzidi kuwapumulia watani zao Simba baada ya leo kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam. 
Kwa matokeo hayo, Yanga imerejea katika nafasi ya pili nyuma ya Simba wakitofautiana pointi tatu pekee huku kila timu ikiwa imeshuka dimbani mara 20.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, timu hizo zilikuwa suluhu na kuwafanya mashabiki wa Yanga kuwa na hofu wakihofia timu yao huenda ikalazimishwa sare.
Kipindi cha pili kilipoanza katika dakika ya 53, Ibrahim Ajib alifunga bao la kwanza kwa njia ya penati, baada ya beki wa Kagera Sugar kuunawa mpira katika eneo la hatari.
Yanga iliendeleza mashambulizi na katika dakika ya 77 Emmanue Martin alifunga bao la pili baada ya pasi nzuri ya Chirwa na kufanya timu hiyo kuwa mbele kwa mabao 2-0.
Kazi nzuri ya Mhilu ilizidi kuzaa matunda tena, ambapo katika dakika ya 88, Godfrey Taita alijifunga, kufuatia kazi nzuri ya Mhilu aliyepiga shuti kali lililosababisha mchezaji huyo wa Kagera kujifunga.
Yanga sasa ina pointi 43 ikiwa nafasi ya pili, huku Simba ikiwa na pointi 46, na Azam imeshuka hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 41.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.