Habari za Punde

HALI YA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NCHINI YAIMARIKA

 Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe (Mb) akitoa maelezo kuhusu hoja mbalimbali zilizowasilishwa kuhusu utoaji huduma ya maji nchini katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb), kulia, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Mhe. January Makamba (Mb) washiriki katika mkutano wa  Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe (Mb) hayupo pichani.
 Kutoka kushoto;  Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembea (Mb), akifuatiwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Mhe. January Makamba (Mb) na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb), wakisikiliza maswali kutoka waandishi wa habari. 
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe (Mb) akitoa maelezo ya ziada kwa vyombo vya habari kuhusu hoja mbalimbali zilizowasilishwa kuhusu utoaji huduma ya maji nchini katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
*******************************************
Serikali imewekeza na kuimarisha upatikanaji wa maji safi kwa wananchi iliyokua asilimia 50 hadi kufikia asilimia 78 mijini na vijijini asilimia 68.8 kwa kutekeleza idadi ya miradi ya maji 1810. 
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe (Mb) amesema hayo leo mjini Dodoma wakati akitoa maelezo kuhusu hoja mbalimbali kuhusu utoaji wa huduma ya maji nchini. 
“ Kutokana na uwekezaji katika kuboresha huduma ya maji safi, hadi kufikia mwezi Disemba 2017 hali ya upatikanaji wa maji mijini ilikuwa asilimia 78 na kwa upande wa vijijini, hadi kufikia mwezi Machi 2018, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ilikuwa imejenga vituo vya kuchotea maji 123,888 vyenye uwezo wa kuhudumia watu milioni zaidi ya 30, sawa na asilimia 85.2” Waziri Kamwelwe amesema na kuongeza vituo vinavyofanya kazi ni 85,286 sawa na asilimia 68.8. 
Waziri Kamwelwe amesema kufuatia hatua hizo matumizi ya maji katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii nayo yameongezeka ambapo taarifa ya Umoja wa Mataifa kuhusu maji ya mwaka 2017 (2017 UN World Water Development Report, Wastewater: The Untapped Resource) inaonesha kuwa asilimia 80 ya maji safi yanayozalishwa na kutumika katika shughuli mbalimbali za kibinadamu hurudi katika mazingira kama majitaka hasa mijini. 
Waziri Kamwelwe akieleza kuhusu mamlaka sita zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amesema katika kipindi cha mwaka 2016/2017 jumla ya lita trioni 1.96 za maji safi zilizalishwa katika mamlaka hizo ambazo baada ya matumizi asilimia 80 ya maji hayo yaligeuka kuwa maji taka. 
Waziri Kamwelwe amempongeza CAG kwa ripoti iliyobaini huduma ya uondoaji majitaka katika miji nchini si ya kuridhisha. Aidha ameongeza kuwa taarifa ya tathmini ya utendaji wa mamlaka za maji ya tarehe 16 Februari 2018 nchini inaonyesha bado huduma hiyo ipo chini ya asilimia 10. 
Waziri Kamwelwe amesema Serikali imeona changamoto hiyo na kuchukua hatua ikiwemo kuweka mipango na mikakati ya kuboresha huduma hiyo ili kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2020, asilimia 30 ya Watanzania wapate hudumu ya uondoaji majitaka. 
Hatua nyingine amesema ni pamoja na kutoa tuzo kwa mamlaka zitakazofanya vizuri katika tathmini ya kila mwaka, kuweka utaratibu kwa kila mradi wa maji safi kuhuisha uondoaji wa majitaka na usafi wa mazingira, kuandaa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kuondoa majitaka na kuandaa Sera mahsusi ya uondoaji wa majitaka na usafi wa mazingira nchini. 
Waziri Kamwelwe amesema mpango huo umezingatia Manispaa ya Dodoma hasa kwa kutambua ongozeko la watu kufuatia serikali kuhamia makao makuu ya nchi ambapo ujenzi wa miundombinu ya uondoaji majitaka unaokadiriwa kugharimu Dola za Marekani milioni 56 utatekelezwa katika mwaka 2019/2020. 
Wizara ya Maji na Umwagiliaji inasimamia mamlaka 25 za maji za miji mikuu ya mikoa ambapo mamlaka sita kati ya hizo zilikaguliwa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kuhusu Ufanisi wa Usimamizi wa Utoaji wa Huduma za Majitaka na Usafi wa Mazingira mijini (Performance Audit Report on Provision of Sewerage Services in Urban Areas). 
Mamlaka zilizokaguliwa ni za miji ya Dar es Salaam (DAWASCO), Dodoma (DUWASSA), Mbeya (Mbeya UWSA), Mwanza (MWAUSSA), Songea (SOUWSSA) na Tanga ( Tanga-UWSA). Taarifa hiyo ilionyesha kuwa kuna hali isiyoridhisha katika utoaji wa huduma ya Uondoaji wa Majitaka katika maeneo ya mjini.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.