Habari za Punde

MVUA YAWAZUIA AZAM FC NA RUVU SHOOTING KUKIPIGA MABATINI

MCHEZO wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya wenyeji, Ruvu Shooting na Azam FC uliokuwa upigwe kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani umeahirishwa hadi kesho Saa 10:00 jioni.
Sababu za kuahirishwa kwa mchezo huo ni maji mengi kutuwama kwenye Uwanja wa Mabatini kutokana na mvua kubwa iliyonyesha leo.
Mechi nyingine mbili za Ligi Kuu zinatarajiwa kuendelea kama kawaida, Simba SC wakiwakaribisha Mbeya City Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam na Mtibwa Sugar wakiwa wenyeji wa Ndanda FC Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Ikumbukwe mechi tano za Ligi Kuu zilichezwa jana kwenye viwanja tofauti, Yanga SC ikilazimishwa sare ya 1-1 na Singida United Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Maji Maji ikiichapa 3-1 Stand United Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Nayo Mbao FC ikishinda 2-1 dhidi ya Njombe Mji FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Mwadui FC iliichapa 2-1 Lipuli ya Iringa Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga wakati Tanzania Prisons ililazimishwa sare ya 1-1 na Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.