Habari za Punde

OFISI YA RAIS-UTUMISHI YAPATA MFANYAKAZI BORA WA MWAKA 2018

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Dorothy Mwaluko akifungua mkutano wa kumchagua mfanyakazi bora wa mwaka 2018 wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora uliofanyika mapema leo katika ofisi hiyo mkoani Dodoma.
*********************************************************
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imefanya uchaguzi wa kumpata mfanyakazi bora wa mwaka 2018 kwa kuwashindanisha wafanyakazi bora kutoka Idara na Vitengo vya ofisi hiyo. 
Mfanyakazi bora aliyechaguliwa ni Bi. Umul-Kher Ally Seiff ambaye ni Afisa Utumishi kutoka Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma. 
Akifungua mkutano huo wa uchaguzi uliofanyika mapema leo katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Rais-Utumishi, Dodoma, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Dorothy Mwaluko aliwataka watumishi kufanya uchaguzi wa haki kwa kumchagua mfanyakazi bora anayestahili na atakayebeba taswira halisi ya ofisi. 
Bi. Mwaluko aliongeza kuwa, mfanyakazi atakayechaguliwa anatakiwa kuwa na sifa ambazo kila anapotazamwa na jamii atoe taswira nzuri ya ofisi. 
Mara baada ya kumtangaza mfanyakazi bora, Bi. Mwaluko amempongeza kwa ushindi na kumtakia heri katika kuitumikia vema dhamana aliyopewa ambayo ni chachu kwa watumishi wengine kiutendaji. 
Kwa upande wake, mfanyakazi bora aliyechaguliwa, Bi. Umul-Kher Ally Seiff amewashukuru watumishi kwa kuona utendaji wake na kumchagua kuwa mfanyakazi bora. Aidha ametoa wito kwa watumishi wote kufanya kazi kwa upendo na ushirikiano kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.
Sehemu ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Dorothy Mwaluko akitoa maelekezo kuhusu uchaguzi wa kumpata mfanyakazi bora wa ofisi wa mwaka 2018.
Wawakilishi wa wafanyakazi bora wa Idara/Vitengo vya Ofisi ya Rais-Utumishi wakishuhudia zoezi la kuhesabu kura ili kumpata mfanyakazi bora wa ofisi wa mwaka 2018.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.