Habari za Punde

SIMBA YAZIDI KUWASHA TAA YA KIJANI KUELEKEA UBINGWA


Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, akiwania mpira na beki wa Mbeya City, Haruna Shamte, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara uliomalizika hivi punde kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Katika mchezo huo Simba ilishinda mabao 3-1 na kufikisha jumla ya Pointi 55. Picha Zote na Muhidin Sufiani (MAFOTO)

 Mshambuliaji wa Simba John Bocco (kulia) akiwatoka mabeki wa Mbeya City, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam,leo. Katika mchezo huo Simba ilishinda mabao 3-1. 
 Kipa na mabeki wa Mbeya City wakichanganyana na kushindwa kuokoa mpira uliopigwa na Emmanuel Okwi aliyefunga bao la pili katika mchezo huo.
***************************************
Na Ripota wa Mafoto Blog, Dar
TIMU ya Simba inaonyesha kukaribia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kutokana na kasi yake ya kufumania nyavu katika kila mchezo.
Simba imeendelea kujiweka karibu na ubingwa baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 kwaenye mechi yake ya raundi ya 23 dhidi ya Mbeya City na kufikisha jumla ya pointi 55 huku ikiwaacha wapinzani wake Yanga wakibaki na Pointi 47.
Simba wamepata ushindi huo leo, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo kwa sasa inaongoza kwa  tofauti ya pointi nane dhidi ya Yanga.
Simba inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 55 baada ya kucheza michezo 23 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 47 baada ya kucheza michezo 22.
Mpira ulianza kwa kasi ya timu zote kushambuliana huku kila timu ikihitaji bao la mapema.
Ilikuwa ni katika dakika ya tano mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya alikosa nafasi ya wazi baada ya kupiga shuti kali lilotoka nje ya goli.
Emmanuel Okwi aliiandikia Simba bao la kwanza katika dakika ya 18 kwa shuti kali akimalizia shuti lilopigwa na John Bocco na kutemwa na kipa wa Mbeya City, Owen Chaima aliutema.
Katika dakika ya 25, mshambuliaji wa Mbeya City, Victor Hangaya alikosa nafasi ya wazi baada ya kupiga shuti akiwa na kipa na kutoka nje kidogo ya goli.
Kwenye dakika ya 31, John Bocco 'Adebayor' akiwa na kipa alikosa nafasi ya wazi ambapo alipiga shuti kali lilopaa pembeni ya goli.
Simba ilipata bao la pili katika dakika ya 34 kupitia kwa beki wake Asante Kwasi ambaye alifunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya Shomari Kapombe kutokea upande wa kulia wa uwanja na kuzamisha mpira wavuni.
Kiungo Frank Ikobela aliipatia bao Mbeya City katika dakika ya 36 akiunganishwa kwa kichwa kona iliyochongwa na Majaliwa Shabani.
Dakika moja baadae, nahodha Bocco aliifungia bao la tatu timu yake ya Simba kwa kichwa akiunganisha krosi ya Kapombe na mkumuacha kipa Chaima akiwa hana la kufanya.
Hadi mwamuzi Mabena anapyenga filimbi ya kuashiria mapumziko, Simba ilikuwa ikiongoza kwa mabao 3-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kushambulia kwa kasi ya hali ya juu ambapo kwenye dakika ya 53, Okwi alikosa nafasi ya wazi akipiga shuti ambalo liligonga mwamba na kutoka nje ya uwanja.
Mbeya City ilifanya mabadiliko ili kuongeza nguvu kwenye dakika ya 61 ambapo ilimtoa Danny Joram na nafasi yake aliingia Mohammed Samata.
Dakika nne baadae Ikobela alikosa nafasi ya wazi baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Hangaya ambapo Aishi Manula alidaka mpira.
Simba ilifanya mabadiliko katika dakika ya 73, alitoka Kwasi na kuingia Tshabalala ambaye alichezewa rafu kwenye dakika ya 74 na Ikobela ambaye alionyeshwa kadi ya njano na mwamuzi Mabena.
Mshambuliaji aliyekuwa msumbufu kwenye ngome ya Simba, Hangaya alifanyiwa mabadiliko katika dakika ya 77 nafasi yake ilichukuliwa na Godfrey Muller.
Bocco alifanyiwa mabadiliko dakika moja baadaye ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Mrundi Laudit Mavugo ambaye hakucheza katika kiwango kizuri.
Mbeya City ilishindwa kupata bao la pili kwenye dakika ya 85, baada ya kiungo Samatta kukosa nafasi ya wazi kwa kichwa akiunganisha krosi ya Ikobela ambapo Manula aliipangua.
Simba: Aishi Manula, Asante Kwasi, Nicholas Gyan, Juuko Murshid, Yusufu Mlipili, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Emmanuel Okwi, John Bocco na Shiza Kichuya.
Mbeya City: Owen Chaima,  Rajabu Isihaka, Majaliwa Shabani, Ally Lundenga, Babu Ally, Ramadhani Malima, Haruna Shamte, Eliud Ambokile, Danny Joram, Victor Hangaya na Frank Ikobela.
 Beki wa Mbeya City, Majaliwa Shaban (kushoto) akichuana kuwania mpira na Shomari Kapombe wa Simba wakati wa mchezo huo.
 Emmenuel Okwi (katikati) akijaribu kuwatoka mabeki wa Mbeya City
 Beki wa Simba, Nichoras Gyan (kulia) akimtoka beki wa Mbeya City, Ally Lundenga, wakati wa mchezo huo

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.