Meneja wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Geita
James Jilala (kulia) akijadiliana jambo na Meneja wa Huduma na Elimu kwa
Mlipakodi kutoka TRA Makao Makuu Gabriel Mwangosi wakati wa kampeni maalum ya
utoaji huduma na elimu kwa mlipakodi iliyomalizika mwishoni mwa wiki mkoani Geita. Katikati ni Afisa wa Kodi
Mwandamizi wa TRA Makao
Makuu Maternus Mallya.
Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakiwasajili wafanyabiashara wapya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wakati wa kampeni maalum ya utoaji huduma na elimu kwa mlipakodi iliyomalizika mwishoni mwa wiki ikiwa na lengo la kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kodi, kusajili wafanyabiashara wapya, pamoja na kusikiliza malalamiko, changamoto na maoni kutoka kwa wafanyabiashara hao.
Afisa wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Lameck Ndida akitoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kodi kwa wafanyabiashara wakati wa kampeni maalum ya utoaji huduma na elimu kwa mlipakodi iliyomalizika mwishoni mwa wiki ikiwa na lengo la kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kodi, kusajili wafanyabiashara wapya, pamoja na kusikiliza malalamiko, changamoto na maoni kutoka kwa wafanyabiashara hao.
*************************************
Na
Veronica Kazimoto, Geita
Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) imesajili jumla ya wafanyabiashara wapya 600 katika kampeni
maalum ya utoaji huduma na elimu kwa mlipakodi iliyofanyika mkoani Geita ikiwa
na lengo la kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kodi pamoja na kusikiliza
malalamiko, changamoto na maoni kutoka kwa wafanyabiashara hao.
Akizungumza mara baada ya
kukamilika kwa kampeni hiyo mwishoni mwa wiki, Menenja wa TRA mkoani hapa James
Jilala ameishukuru Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa kufika mkoani Geita
hususani katika maeneo ambayo hakuna ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania na
kufanikiwa kusajili wafanyabiashara wengi ndani ya wiki moja.
"Nianze kwa
kuishukuru Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa hatua ambayo mmeifanya ya
kufika katika Mkoa wetu wa Geita hasa maeneo ambayo hatuna ofisi ya TRA na kufanikiwa kusajili wafanyabiashara wengi kwa
muda mfupi kitu ambacho kimekuwa historia kwetu," alisema Jilala.
Jilala alisema kuwa,
baadhi ya wafanyabiashara walishindwa kusajiliwa na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa
wakati, kwasababu walitakiwa kusafiri zaidi ya kilomita 100 kwenda Geita mjini
kwa ajili ya kupata huduma hiyo. Hivyo, zoezi hili limewarahisishia
wafayabiashara kusajiliwa na kupatiwa TIN.
Naye Meneja wa Huduma na
Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Makao Makuu
Gabriel Mwangosi alisema kuwa , pamoja na usajili wa wafanyabiashara hao,
shughuli mbalimbali zimefanyika katika kampeni hiyo ikiwa ni pamoja na utoaji
wa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu masuala mbalimbali ya kodi kupitia semina
na kuwatembelea katika sehemu zao za biashara.
"Katika zoezi hili
tumefanya shughuli nyingi sana ikiwa ni pamoja na kuwatembelea wafanyabiashara
mahali wanapofanyia biashara zao, tumesajili wafanyabiashara wapya na tumetoa
semina mbalimbali ambazo tunaamini
kabisa zitakuwa zimebadilisha mtizamo,
utendaji na mwenendo mzima wa ulipaji kodi katika Mkoa huu wa Geita,"
alieleza Mwangosi.
Kampeni ya huduma na elimu
kwa mlipakodi ni moja ya mikakati ambayo Mamlaka ya Mapato Tanzania imejiwekea
katika kuhakikisha kuwa inasajili wafanyabiashara 1,000,000 katika mwaka huu wa
Fedha wa 2017/18.
No comments:
Post a Comment